YouVersion Logo
Search Icon

1 Mambo ya Nyakati UTANGULIZI

UTANGULIZI
Vitabu viwili viitwavyo “Mambo ya Nyakati” vyaweza kufikiriwa kama kitu kimoja. Vyote kwa jumla ni kumbukumbu ya historia ambayo inaeleza kwa namna ya pekee habari za watu wa Israeli, watu wa Mungu, tangu mwanzo wao mpaka wakati wa kupelekwa kwa watu wa Israeli uhamishoni Babuloni.
Visa hivi vya historia havisimuliwi tu kama historia, bali vinaelezwa kutokana na fikira na hisia za kidini. Mwandishi anatumia habari za matukio yaliyokuwako kabla ya nyakati zake, kama zile za Samueli na vitabu vya Wafalme, lakini uchaguzi wake wa kuzitaja habari hizo waonekana wazi kwamba alikuwa anataka hasa kukaza mafundisho ya matukio hayo: Mungu mwenyewe ndiye mtawala wa watu wa Israeli; wafalme wa Israeli ni watumishi tu waliopewa jukumu na mamlaka ya kuwaonesha watu uwezo wake Mungu katika maisha yao. Miongoni mwa hao wafalme Daudi ndiye aliyefana kupita wote kwa uaminifu. Daudi ndiye aliyewahi kumiliki mji wa Yerusalemu ambao baadaye ulipata kuwa mji mtakatifu kwa sababu ya kuweko humo hekalu la Mungu. Daudi ndiye aliyepata kuongoza maisha ya kiraia na ya kidini ya watu wa Israeli.
Kitabu chenyewe kinagawanyika katika sehemu mbili kuu:
Sehemu ya kwanza (sura 1-9) mwandishi anatupa orodha ya nasaba kuanzia Adamu mpaka wakati Waisraeli waliporudi kutoka uhamishoni kule Babuloni. Orodha hiyo aghalabu ina shabaha ya kuonesha kwamba Waisraeli wanaungana na historia ya wazee kiungo chao kikiwa ni Daudi.
Sehemu ya pili (sura 10-29) inahusu hasa historia ya utawala wa Daudi. Lakini mwandishi ameacha visa ambavyo havioneshi ukuu wa utawala wake kama vile ugomvi wake na Sauli, utawala wake wa miaka saba kule Hebroni, kisa kile cha Bathsheba na kukosolewa na nabii Nathani, uasi wa Absalomu, n.k. Badala yake, mwandishi anazingatia vile visa ambavyo vinaonesha jinsi Daudi alivyochangia kufana kwa utawala wa Waisraeli hata kufikia ufanisi wa ibada kwa Mwenyezi-Mungu: Kurudishwa kwa sanduku la agano, kuhesabiwa kwa watu ambako kunachukuliwa kuwa ni jambo lisilofaa, na mwishowe mpango wa vikundi mbalimbali ambavyo vitahusika katika huduma ya hekalu: Makuhani, walawi, wangoja mlango, n.k.
Kitabu hiki labda kiliandikwa mwishoni mwa karne ya sita K.K. na mtu ambaye bila shaka alikuwa wa kundi la makuhani wa ukoo wa Lawi.

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy