Mwanzo 33
33
Yakobo anakutana na Esau
1Basi, Yakobo akainua macho, akamwona Esau akikuja pamoja na watu mia ine. Halafu, akawagawanya watoto wake kati ya Lea, Rakeli na wale wajakazi wawili. 2Akawaweka wajakazi na watoto wao mbele, kisha Lea na watoto wake, na nyuma kabisa wakafuata Rakeli na mwana wake Yosefu. 3Kisha yeye mwenyewe akawatangulia. Akakwenda akiinama uso mpaka chini kwa heshima mara saba, mpaka alipofika karibu na ndugu yake.
4Basi, Esau akakwenda mbio kumupokea Yakobo, akamukumbatia, kumubusu kwenye shingo, na wote wawili wakalia. 5Esau alipoinua macho na kuwaona wale wamama na watoto, akauliza: “Ni wa nani hawa unaokuwa nao?”
Yakobo akamujibu: “Hawa ni watoto ambao Mungu, kwa neema yake, amenijalia mimi mutumishi wako.”
6Kisha wale wajakazi wakakaribia pamoja na watoto wao, wakainama kwa heshima. 7Vilevile Lea akakuja pamoja na watoto wake, akainama kwa heshima. Kwa mwisho Rakeli na Yosefu wakakuja, wakainama kwa heshima.
8Halafu Esau akauliza: “Kundi lile nililokutana nalo katika njia lina maana gani?”
Yakobo akamujibu: “Nilitumaini kupata kukubaliwa mbele yako, ee bwana wangu.”
9Lakini Esau akasema: “Nina mali ya kutosha, ndugu yangu. Mali yako ikuwe yako mwenyewe.”
10Yakobo akamwambia: “Hapana! Kama kweli nimekubaliwa mbele yako, ninakusihi uipokee zawadi yangu. Hakika, kuona uso wako ni kama kuona uso wa Mungu, kwa vile ulivyonipokea kwa wema mukubwa. 11Basi, ninakuomba ukubali zawadi niliyokuletea, kwa sababu hata mimi vilevile Mungu amenineemesha, nami nina mali nyingi.” Ndivyo Yakobo alivyomushawishi Esau, naye akapokea zawadi yake.
12Esau akasema: “Basi! Tuendelee na safari yetu. Mimi nitakutangulia.”
13Lakini Yakobo akamwambia: “Bwana wangu, wewe unajua kwamba watoto hawa ni wachanga, na kwamba nyama hawa wananyonyesha, nami ninapaswa kuwatunza. Kama nyama hawa watapelekwa mbio kwa siku moja, wote watakufa. 14Basi, ninakuomba utangulie, nami nitafuata polepole kadiri ya mwendo wa nyama na watoto, mpaka nitakapokufikia kule Seiri.”
15Esau akasema: “Heri nikuachie sehemu ya watu wangu.”
Lakini Yakobo akasema: “Kuna sababu gani ya kufanya hivyo? Inanitosha kwamba mimi nimepata kukubaliwa mbele yako, ewe bwana wangu.” 16Basi, siku hiyo Esau akaanza safari ya kurudi Seiri. 17Lakini Yakobo akasafiri kwenda Sukoti, na kule akajijengea nyumba na vibanda kwa ajili ya nyama wake. Kwa sababu hiyo, pahali hapo pakaitwa Sukoti, ni kusema “Vibanda”.
18Kutoka Padani-Aramu, Yakobo akafika salama kwa muji wa Sekemu, katika inchi ya Kanana, akapiga kambi yake karibu na muji ule. 19Sehemu hiyo ya inchi ambako alipiga kambi aliinunua kutoka kwa wazao wa Hamori, baba ya Sekemu, kwa vikoroti mia moja vya feza. 20Basi, akajenga mazabahu pahali pale na kuiita “Mungu ni Mungu wa Israeli”.
Currently Selected:
Mwanzo 33: SWC02
Highlight
Share
Copy

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Bible in Swahili Congo © Bible Society of the Democratic Republic of Congo (DRC), 2002.