YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 119

119
Utukufu wa sheria ya Mungu
1 # Zab 128:1 Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya BWANA.
2 # Kum 4:29 Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
3 # Rum 7:16,17; 1 Yoh 3:9 Naam, hawakutenda ubatili,
Wamekwenda katika njia zake.
4Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
5 # Yer 31:33; Rum 7:22,23; 2 Kor 3:5 Ningependa njia zangu ziwe thabiti,
Nizitii amri zako.
6 # Ayu 22:26; 1 Yoh 2:28 Ndipo mimi sitaaibika,
Nikiyaangalia maagizo yako yote.
7Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,
Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako.
8Nitazitii amri zako,
Usiniache kabisa.
* * *
9 # Mit 1:4,10 Jinsi gani kijana aisafishe njia yake?
Kwa kutii, akilifuata neno lako.
10 # 2 Nya 15:15 Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
11 # Lk 2:19 Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
Nisije nikakutenda dhambi.
12Ee BWANA, umehimidiwa,
Unifundishe amri zako.
13Kwa midomo yangu nimezisimulia
Hukumu zote za kinywa chako.
14Nimeifurahia njia ya shuhuda zako
Kana kwamba ni mali mengi.
15 # Zab 1:2 Nitayatafakari maagizo yako,
Na kuziangalia njia zako.
16Nitajifurahisha sana kwa amri zako,
Sitalisahau neno lako.
* * *
17Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
18Unifumbue macho yangu niyatazame
Maajabu yatokayo katika sheria yako.
19 # Mwa 47:9; Ebr 11:13 Mimi ni mgeni katika nchi,
Usinifiche maagizo yako.
20Roho yangu imepondeka kwa kutamani
Hukumu zako kila wakati.
21Umewakemea wenye kiburi,
Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.
22Uniondolee laumu na dharau,
Kwa maana nimezishika shuhuda zako.
23Wakuu nao waliketi wakaninena,
Lakini mtumishi wako atazitafakari amri zako.
24Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu.
* * *
25 # Zab 143:11 Nafsi yangu imegandamia mavumbini,
Unihuishe sawasawa na neno lako.
26 # 1 Fal 8:36; Zab 27:11 Nilizisimulia njia zangu ukanijibu,
Unifundishe amri zako.
27Unifahamishe njia ya maagizo yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako.
28Nafsi yangu imeyeyuka kwa huzuni,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako.
29 # Mit 30:8; Ebr 8:10 Uniondolee njia ya uongo,
Unineemeshe kwa sheria yako.
30Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
31Nimeambatana na shuhuda zako,
Ee BWANA, usiniaibishe.
32 # 1 Fal 4:29; Isa 60:5; 2 Kor 6:11 Nitakwenda mbio katika njia ya maagizo yako,
Utakaponipanulia ufahamu wangu.
* * *
33 # Mt 10:22; Ufu 2:26 Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako,
Nami nitaishika hadi mwisho.
34 # Mit 2:6; Yak 1:5 Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
35Uniendeshe katika mapito ya amri zako,
Kwa maana nimependezwa nayo.
36 # Eze 33:31; Mk 7:21; Lk 12:15; 1 Tim 6:10; Ebr 13:5 Unielekeze moyo wangu katika shuhuda zako,
Wala usiielekee tamaa.
37 # Ayu 31:1 Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa,
Unihuishe katika njia yako.
38 # 2 Sam 7:25 Umthibitishie mtumishi wako ahadi yako,
Iliyo ya wanaokucha.
39Uniondolee laumu niiogopayo,
Maana hukumu zako ni njema.
40Tazama, nimeyatamani mausia yako,
Unihuishe kwa haki yako.
* * *
41Ee BWANA, fadhili zako zinifikie na mimi,
Naam, wokovu wako kulingana na ahadi yako.
42Nami nitamjibu neno anilaumuye,
Kwa maana nilitumainia neno lako.
43Usiliondoe neno la kweli kinywani mwangu kamwe,
Maana nimezingojea hukumu zako.
44Nami nitaitii sheria yako daima,
Naam, milele na milele.
45 # Yn 8:32,36; Rum 8:2 Nami nitakwenda kwa uhuru,
Kwa kuwa nimejifunza mausia yako.
46 # Mt 10:18; Mdo 26:1,2 Nitazinena shuhuda zako mbele ya wafalme,
Wala sitaona aibu.
47Nami nitajifurahisha sana kwa maagizo yako,
Ambayo nimeyapenda.
48Na mikono yangu nitayainulia maagizo yako niliyoyapenda,
Nami nitazitafakari amri zako.
* * *
49Likumbuke neno ulilomwambia mtumishi wako,
Ambalo kwalo umenipa tumaini.
50 # Zab 27:13; Yer 15:16; Rum 5:3-5; Ebr 6:17-19 Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu,
Ya kwamba ahadi yako imenipa moyo.
51 # Yer 20:7; Ayu 23:11 Wenye kiburi wamenidharau mno,
Lakini sikiuki sheria zako.
52Ninapozikumbuka hukumu zako za tangu kale,
Ee BWANA, ninafarijika.
53 # Ezr 9:3 Ghadhabu kuu imenishika kwa sababu ya wasio haki,
Waiachao sheria yako.
54Amri zako zimekuwa nyimbo zangu,
Katika nyumba yangu ya ugenini.
55 # Zab 63:6 Wakati wa usiku nimelikumbuka jina lako,
Ee BWANA, nikaitii sheria yako.
56Hayo ndiyo niliyokuwa nayo,
Kwa sababu nimeyashika mausia yako.
* * *
57 # Zab 16:5; Yer 10:16; Omb 3:24 BWANA ndiye aliye fungu langu,
Ninaahidi kuyatii maneno yake.
58Nimekuomba radhi kwa moyo wangu wote,
Unifadhili kulingana na ahadi yako.
59 # Omb 3:40; Yoe 2:13; Lk 15:17 Ninapozitafakari njia zako,
Naielekeza miguu yangu kwa shuhuda zako.
60Nilifanya haraka wala sikukawia,
Kuyatii maagizo yako.
61Japo kamba za wasio haki zimenifunga,
Siisahau sheria yako.
62 # Mdo 16:25 Usiku wa manane nitaamka nikushukuru,
Kwa sababu ya hukumu zako za haki.
63Mimi ni mwenzi wa watu wote wakuchao,
Na wale wayatiio mausia yako.
64 # Zab 33:5 BWANA, dunia imejaa fadhili zako,
Unifundishe amri zako.
* * *
65Umemtendea mtumishi wako mema,
Ee BWANA, sawasawa na neno lako.
66Unifundishe akili na maarifa,
Maana nimeyaamini maagizo yako.
67 # Kum 32:15; Yer 31:18; Hos 5:15; Ebr 12:11; Ufu 3:19 Kabla sijateswa mimi nilipotea,
Lakini sasa nimelitii neno lako.
68 # Kut 34:6; Zab 107:1; Mt 19:7 Wewe U mwema na mtenda mema,
Unifundishe amri zako.
69 # Ayu 13:4 Wenye kiburi wamenizulia uongo,
Lakini kwa moyo wangu wote nitayashika mausia yako.
70 # Mdo 28:27 Mioyo yao imenenepa kama shahamu,
Lakini mimi nimeifurahia sheria yako.
71 # Ebr 12:10; Mit 8:10 Ilikuwa vema kwangu kuwa niliteswa,
Nipate kujifunza amri zako.
72Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
* * *
73 # Ayu 10:8; Zab 100:3 Mikono yako iliniumba na kunidhibiti,
Unifahamishe nikajifunze amri zako.
74 # Zab 34:2 Wakuchao na wanione na kufurahi,
Kwa sababu nimelitumainia neno lako.
75 # Zab 89:30-33; Ebr 12:10 Najua ya kuwa hukumu zako ni za haki,
Ee BWANA, na kwa uaminifu umenitesa.
76Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu,
Kulingana na ahadi yako kwa mtumishi wako.
77Rehema zako zinijie nipate kuishi,
Maana sheria yako ni furaha yangu.
78 # Zab 25:3 Wenye kiburi waaibike, maana wamenidhulumu kwa uongo,
Mimi nitayatafakari mausia yako.
79Wakuchao na wanirudie,
Nao watazijua shuhuda zako.
80 # 2 Nya 15:7; Mit 4:23; Yn 1:47 Moyo wangu na uwe mkamilifu katika amri zako,
Nisije mimi nikaaibika.
* * *
81 # Zab 42:1,2; 73:26 Nafsi yangu imefifia kwa kuutamani wokovu wako,
Nimelitumainia neno lako.
82 # Zab 69:3 Macho yangu yamefifia kwa kuitazamia ahadi yako,
Nikisema, Lini utakaponifariji?
83 # Ayu 30:30 Maana nimekuwa kama kiriba katika moshi,
Sikuzisahau amri zako.
84 # Zab 39:4; 7:6; Ufu 6:10 Siku za mtumishi wako ni ngapi,
Lini utakapowahukumu wale wanaonifuatia?
85 # Zab 35:7 Wenye kiburi wamenichimbia mashimo,
Ambao hawaifuati sheria yako.
86 # Zab 7:1-5; 35:19 Amri zako zote ni za kudumu,
Ninateswa bila sababu, nisaidie!
87Walikuwa karibu na kunikomesha katika nchi,
Lakini sikuyaacha mausia yako.
88Uniponye kwa fadhili zako,
Nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.
* * *
89 # Mt 5:18; 1 Pet 1:25 Ee BWANA, neno lako lasimama
Imara mbinguni hata milele.
90Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi,
Umeiweka nchi, nayo imethibitika.
91 # Mwa 8:22; Zab 148:6; Yer 33:25 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo,
Maana vitu vyote ni watumishi wako.
92 # Rum 15:4 Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu,
Hapo ningalipotea katika mateso yangu.
93Hata milele sitayasahau maagizo yako,
Maana kwa hayo umenihuisha.
94 # Hos 2:7,16 Mimi ni wako, uniokoe,
Kwa maana nimejifunza mausia yako.
95Wasio haki wameniotea ili kunipoteza,
Nitazitafakari shuhuda zako.
96 # Isa 40:8; Mt 5:18 Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho,
Bali amri yako haina kikomo.
* * *
97 # Zab 1:2 Sheria yako naipenda mno ajabu,
Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.
98 # Kum 4:6,8; Isa 48:17 Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu,
Kwa maana ninayo sikuzote.
99 # 2 Tim 3:15 Ninazo akili kuliko waalimu wangu wote,
Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo.
100 # Ayu 12:12; 32:7 Ninao ufahamu kuliko wazee,
Kwa kuwa nimeyashika mausia yako.
101 # 2 Kor 7:1; Mit 1:15 Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya,
Ili nilitii neno lako.
102Sikuziacha hukumu zako,
Maana Wewe mwenyewe umenifundisha.
103 # Zab 19:10; Mit 8:11 Mausia yako ni matamu sana kwangu,
Kupita asali kinywani mwangu.
104Kwa mausia yako najipatia ufahamu,
Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo.
* * *
105Neno lako ni taa ya miguu yangu,
Na mwanga wa njia yangu.
106 # Neh 10:29 Nimeapa nami nikathibitisha,
Kuzishika hukumu zako za haki.
107Nimeteswa mno;
Ee BWANA, unihuishe sawasawa na neno lako.
108 # Hos 14:2; Ebr 13:15 Ee BWANA, uziridhie sadaka za kinywa changu,
Na kunifundisha hukumu zako.
109 # Amu 12:3; Ayu 13:14 Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima,
Lakini sheria yako sikuisahau.
110Watendao uovu wamenitegea mtego,
Lakini sitoki katika njia ya mausia yako.
111 # Kum 33:4 Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
Maana ndizo changamko la moyo wangu.
112Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako,
Daima, naam, hata milele.
* * *
113Watu wa kusitasita nawachukia,
Lakini sheria yako naipenda.
114 # Zab 32:7 Ndiwe sitara yangu na ngao yangu,
Neno lako nimelingojea.
115 # Zab 6:8; Mt 7:23 Enyi watenda mabaya, ondokeni kwangu,
Niyashike maagizo ya Mungu wangu.
116 # Zab 25:2; Rum 5:5; 9:33 Unitegemeze kulingana na ahadi yako, nikaishi,
Wala usiniache niyaaibikie matumaini yangu.
117 # Zab 71:6; Yn 10:28; Rum 14:4 Unisaidie nami nitakuwa salama,
Nami nitaziangalia amri zako daima.
118Umewakataa wote wazikosao amri zako,
Kwa maana hila zao ni bure.
119 # Eze 22:18 Wabaya wa nchi pia umewaondoa kama takataka,
Ndiyo maana nimezipenda shuhuda zako.
120 # Hab 3:16 Mwili wangu unatetemeka kwa kukucha Wewe,
Nami ninaziogopa hukumu zako.
* * *
121Nimefanya hukumu na haki,
Usiniache mikononi mwao wanaonionea.
122 # Ebr 7:22 Uwe mdhamini wa mtumishi wako, apate mema,
Wenye kiburi wasinionee.
123Macho yangu yanafifia kwa kuungojea wokovu wako,
Na kutimizwa kwa ahadi yako ya haki.
124Kama zilivyo rehema zako umtendee mtumishi wako,
Na amri zako unifundishe.
125Mimi ni mtumishi wako, unifahamishe,
Nipate kuzijua shuhuda zako.
126Wakati umewadia BWANA atende kazi;
Kwa kuwa wameitangua sheria yako.
127 # Zab 19:10; Efe 3:8; Mit 3:13,18; 8:11 Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako,
Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.
128Maana nayafuata mausia yako yote, kuwa ya adili,
Kila njia ya uongo naichukia.
* * *
129Shuhuda zako ni za ajabu,
Ndiyo maana roho yangu imezishika.
130 # Zab 19:11; Mit 1:4; 2 Pet 1:19 Kufafanuliwa kwa maneno yako kunatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga.
131Nafunua kinywa changu nikihema,
Maana nazitamani amri zako.
132 # Kut 4:31; 1 Sam 1:11; Zab 106:4 Unigeukie na kunirehemu,
Kama ilivyo desturi yako kwa walipendalo jina lako.
133 # Rum 6:12 Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako,
Uovu usije ukanimiliki.
134 # Lk 1:74 Unikomboe kutoka kwa dhuluma ya mwanadamu,
Nipate kuyashika mausia yako.
135 # Zab 4:6 Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Na kunifundisha amri zako.
136 # Yer 9:1 Macho yangu yachuruzika mito ya machozi,
Kwa sababu hawaitii sheria yako.
* * *
137 # Neh 9:33; Yer 12:1; Dan 9:7 Ee BWANA, Wewe ndiwe mwenye haki,
Na hukumu zako ni za adili.
138Umeziagiza shuhuda zako kwa haki,
Na kwa uaminifu mwingi.
139Juhudi yangu imeniangamiza,
Maana watesi wangu wameyasahau maneno yako.
140Neno lako limesafika sana,
Kwa hiyo mtumishi wako amelipenda.
141 # Mit 15:16; Amo 7:2; Lk 6:20; 2 Kor 8:9; Yak 2:5 Mimi ni mdogo, nadharauliwa,
Lakini siyasahau mausia yako.
142 # Zab 19:9; Yn 17:17; Efe 1:13 Haki yako ni haki ya milele,
Na sheria yako ni kweli.
143Taabu na dhiki zimenipata,
Maagizo yako ni furaha yangu.
144Haki ya shuhuda zako ni ya milele,
Unifahamishe, nami nitaishi.
* * *
145Nimeita kwa moyo wangu wote; Ee BWANA, uitike;
Nitazishika amri zako.
146Nimekuita Wewe, uniokoe,
Nami nitazishika shuhuda zako.
147Naamka kabla ya mapambazuko na kukuomba msaada,
Naweka tumaini langu katika maneno yako.
148 # Zab 63:1,6 Nakaa macho usiku kucha,
Ili kuitafakari ahadi yako.
149Kwa fadhili zako uisikie sauti yangu,
Ee BWANA, uniokoe.
150Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki,
Wamekwenda mbali na sheria yako.
151 # Zab 145:18 Ee BWANA, Wewe U karibu,
Na maagizo yako yote ni kweli.
152 # Lk 21:33 Tokea zamani nimejua kwa shuhuda zako,
Ya kuwa umeziweka zikae milele.
* * *
153 # Omb 5:1 Uyaangalie mateso yangu, uniokoe,
Maana sikuisahau sheria yako.
154 # 1 Sam 24:15; Zab 35:1; Mik 7:9 Unitetee na kunikomboa,
Unihuishe sawasawa na ahadi yako.
155 # Ayu 5:4 Wokovu u mbali na wasio haki,
Kwa maana hawajifunzi amri zako.
156Ee BWANA, rehema zako ni nyingi,
Unihuishe sawasawa na hukumu zako.
157Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi,
Lakini mimi sikiuki shuhuda zako.
158Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa,
Kwa sababu hawakulitii neno lako.
159Uangalie niyapendavyo mausia yako,
Ee BWANA, unihuishe sawasawa na fadhili zako.
160Jumla ya neno lako ni kweli,
Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.
* * *
161 # 1 Sam 24:11 Wakuu wameniudhi bure,
Ila moyo wangu unakaa kwa kicho cha maneno yako.
162Naifurahia ahadi yako,
Kama apataye mateka mengi.
163Nimeuchukia uongo, umenikirihi,
Sheria yako nimeipenda.
164Mara saba kila siku nakusifu,
Kwa sababu ya hukumu za haki yako.
165 # Mit 3:2; Isa 32:17 Wana amani nyingi waipendao sheria yako,
Wala hawana la kuwakwaza.
166Ee BWANA, nimeungojea wokovu wako,
Na maagizo yako nimeyatenda.
167Nafsi yangu imezishika shuhuda zako,
Nami nazipenda mno.
168 # Ayu 34:21; Mit 5:21 Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako,
Maana njia zangu zote ziko mbele zako.
* * *
169Ee BWANA, kilio changu na kikufikie,
Unifahamishe sawasawa na neno lako.
170Dua yangu na ifike mbele zako,
Uniponye sawasawa na ahadi yako.
171Midomo yangu na itoe sifa,
Kwa kuwa unanifundisha mausia yako.
172Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako,
Maana maagizo yako yote ni ya haki.
173 # Yos 24:22; Mit 1:29; Lk 10:42 Mkono wako na uwe tayari kunisaidia,
Maana nimeyachagua mausia yako.
174Ee BWANA, nimeutamani wokovu wako,
Na sheria yako ndiyo furaha yangu.
175Nafsi yangu na iishi, ipate kukusifu,
Na hukumu zako zinisaidie.
176 # Isa 53:6; Mt 10:6; Lk 15:4; 1 Pet 2:25; Eze 34:6; Mt 18:11 Nimetangatanga kama kondoo aliyepotea;
Umtafute mtumishi wako;
Kwa maana sikuyasahau maagizo yako.

Currently Selected:

Zaburi 119: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy