YouVersion Logo
Search Icon

Matendo 18

18
Paulo katika Korintho
1Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho. 2#Rum 16:3 Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Priskila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafika kwao; 3#Mdo 20:34; 1 Kor 4:12 na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. 4Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki.
5 # Mdo 17:14,15 Hata Sila na Timotheo walipoteremka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo. 6#Mdo 13:46,51; 20:26 Walipopingana naye na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. 7Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi. 8#1 Kor 1:14 Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa. 9#1 Kor 2:3 Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, 10#Yos 1:5,9; Isa 41:10; 43:5; Yer 1:8; Hos 2:23; Yn 10:16 kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu. 11Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu.
12Hata Galio alipokuwa mtawala wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, 13wakisema Mtu huyu huwashawishi watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria. 14#Mdo 25:18-20 Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi; 15#Yn 18:31 bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo. 16Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu. 17#1 Kor 1:1 Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu.
Paulo arudi Antiokia
18 # Hes 6:9,18; Mdo 21:24 Baada ya hayo Paulo akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu; na Priskila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri. 19Wakafika Efeso, akawaacha huko. Yeye mwenyewe akaingia katika sinagogi, akahojiana na Wayahudi. 20Walipomtaka akae muda mrefu zaidi, hakukubali; 21#Rum 1:10; 1 Kor 4:19; Yak 4:15 bali aliagana nao, akisema, Nitarejea kwenu tena, Mungu akinijalia. Akatweka, akatoka Efeso, 22#Mdo 21:15 na alipokwisha kushuka Kaisaria, akapanda juu, akawasalimu kanisa, kisha akateremka kwenda Antiokia. 23Baada ya kukaa huko kwa siku kadhaa akaondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji, akiwatia moyo wanafunzi.
Huduma ya Apolo
24 # 1 Kor 3:6 Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, msemaji mzuri, akafika Efeso; naye alikuwa na ujuzi wa Maandiko. 25#Mdo 19:3; Rum 12:11; Ufu 3:15 Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa bidii habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. 26Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Priskila na Akila walipomsikia wakampeleka kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. 27#2 Kor 3:1; Kol 4:10 Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. 28#Mdo 9:22; 17:3 Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionesha kwa maneno ya Maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.

Currently Selected:

Matendo 18: SRUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy