YouVersion Logo
Search Icon

Mk UTANGULIZI

UTANGULIZI
Wataalamu wengi wa mambo ya Biblia wanafikiri Injili hii iliandikwa kabla ya zile Injili nyingine tatu. Mapokeo ya kale yanasema Marko ndiye mwandishi wa injili hii (Marko anatajwa katika Matendo 12:12; 15:37) na anasemekana aliiandika akiwa Rumi kama muhtasari wa mahubiri ya mtume Petro (linganisha 1 Pet 5:13). Ingawa haijulikani kwa hakika wakati ilipoandikwa, maneno ya mwandishi katika 10:30 “pamoja na mateso” ambayo hayamo katika Mathayo au Luka, yanadokezea kwamba mwandishi aliandika wakati Wakristo walipokuwa wanateswa mara baada ya ule moto mkubwa ulioteketeza nusu ya mji wa Roma mnamo mwaka wa 64 B.K. Injili hii inafikiriwa pia kwamba ilitumiwa na waandishi wengine wa injili, yaani Mathayo na Luka, wakati walipoandika habari zao juu ya Yesu Kristo.
Kwa ufupi Marko anatupa picha ya Yesu kama “Mwana wa Mungu” (1:1; rejea pia 1:11; 3:11; 5:7; 9:7; 14:61-62; 15:39) ambaye huduma yake iliandamana na vitendo vilivyoonesha, kwa wale waliokuwa na macho ya kuona, kuweko kwa nguvu ya Mungu na ufalme wake miongoni mwa watu.
Marko aliandika maneno ya Yesu kwa ufupi kuliko waandishi wengine wa injili; injili yake ina mkusanyo mmoja wa maneno ya Yesu kwa mtindo wa mazungumzo (sura 13) na mifano michache (kama vile katika sura 4). Sehemu kubwa za kitabu hiki ni kama ifuatavyo:
1. 1:1-13 Mwanzo wa matukio ya maisha ya Yesu hadharani (habari za Yohana Mbatizaji; ubatizo wa Yesu na kujaribiwa kwake);
2. 1:14–9:50 Mahubiri ya Yesu, mafundisho na huduma yake ya kuponya wagonjwa kule Galilaya.
3. Sura 10 Safari kwenda Yerusalemu.
4. Sura 11–15 Juma la mwisho ambalo linamalizia na kusulibiwa na kuzikwa kwake.
5. 16:1-8 Kufufuka kwake. Kama ilivyo mwanzoni Marko alitangaza kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu (1:1), karibu na mwisho wa injili yake, kana kwamba mwandishi alitaka kufunga habari zake, askari mmoja anarudia maneno yale yale yaliyotangazwa: “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu”.
Hati nyingine za mkono za kale zinaongeza mwishoni mwa sura 16:8 habari ambazo zinarudia baadhi ya visa vya Yesu aliyefufuka kuwatokea wanafunzi wake na pia habari za kupaa kwake mbinguni. Habari hizo zinaelezwa kinaganaga katika injili zile nyingine.

Currently Selected:

Mk UTANGULIZI: SUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy