YouVersion Logo
Search Icon

Lk 1

1
1Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu, 2#Yn 15:27kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo, 3#Mdo 1:1nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu, 4upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.
Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji Kwatabiriwa
5 # 1 Nya 24:10 Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. 6Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. 7Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.
8Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu, 9#Kut 30:7kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. 10Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba. 11Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. 12Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. 14Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake. 15#Hes 6:3; Amu 13:4,5; 1 Sam 1:11Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye. 16Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. 17#Mal 3:1; 4:5-6; Mt 17:11-13Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa. 18#Mwa 18:11Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. 19#Dan 8:16; 9:21; Ebr 1:14Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. 20#Lk 1:45Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.
21Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni. 22Alipotoka hali hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu. 23Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake. 24Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, 25#Mwa 30:23Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.
Kuzaliwa kwa Yesu Kwatabiriwa
26Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, 27#Mt 1:16,18; Lk 2:5kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. 28#Amu 5:24Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. 29Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? 30Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. 31#Mt 1:21-23; Amu 13:3; Isa 7:14Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. 32#2 Sam 7:12,13,16; Isa 9:7Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. 33#Mik 4:7; Dan 7:14Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. 34Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? 35#Kut 13:12; Mt 1:18,20Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. 36Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; 37#Mwa 18:14kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. 38Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Mariamu Amtembelea Elisabeti
39Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, 40akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. 41#Lk 1:15; Mwa 25:22Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; 42#Kum 28:9; Amu 5:24akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. 43Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? 44Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. 45#Lk 1:20; 11:28Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.
Wimbo wa Sifa wa Mariamu
46 # 1 Sam 2:1-10 Mariamu akasema,
Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
47Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;
48 # 1 Sam 1:11; Lk 1:25; Zab 113:5,6; Lk 11:27 Kwa kuwa ameutazama
Unyonge wa mjakazi wake.
Kwa maana, tazama, tokea sasa
Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;
49 # Zab 111:9 Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,
Na jina lake ni takatifu.
50 # Zab 103:13,17 Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi
Kwa hao wanaomcha.
51 # Zab 89:10; 2 Sam 22:28 Amefanya nguvu kwa mkono wake;
Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
52 # Ayu 5:11; 12:19; Zab 147:6; 1 Sam 2:7 Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi;
Na wanyonge amewakweza.
53 # 1 Sam 2:5; Zab 34:10; 107:9 Wenye njaa amewashibisha mema,
Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.
54 # Isa 41:8; Zab 98:3 Amemsaidia Israeli, mtumishi wake;
Ili kukumbuka rehema zake;
55 # Mwa 17:7; 18:18; 22:17; Mik 7:20 Kama alivyowaambia baba zetu,
Ibrahimu na uzao wake hata milele.
56Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.
Kuzaliwa kwa Yohana Mbatizaji
57Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. 58Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. 59#Law 12:3; Mwa 17:12Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. 60#Lk 1:13Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. 61Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. 62Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. 63Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. 64Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. 65Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. 66Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
Unabii wa Zekaria
67Na Zakaria, baba yake, akajazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema,
68 # Lk 7:16; Zab 41:13; 72:18 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa.
69 # 1 Sam 2:10; Zab 18:2; 132:17 Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
70Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;
71 # Zab 106:10 Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
72 # Zab 105:8; 106:45; Mwa 17:7; Law 26:42 Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu;
73 # Mwa 22:16,17; Mik 7:20 Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
74 # Tit 2:12,14 Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
75Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote.
76 # Mal 3:1; Mt 3:3 Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu,
Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake;
77 # Yer 31:34 Uwajulishe watu wake wokovu,
Katika kusamehewa dhambi zao.
78 # Hes 24:17; Isa 60:1,2; Mal 4:2 Kwa njia ya rehema za Mungu wetu,
Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia,
79 # Isa 9:2; 58:8; Mt 4:16 Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti,
Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.
80 # Mt 3:1 Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.

Currently Selected:

Lk 1: SUV

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy