Zaburi 32
32
Zaburi 32
Furaha ya msamaha
Zaburi ya Daudi. Funzo.
1 Heri mtu aliyesamehewa makosa yake,
ambaye dhambi zake zimefunikwa.
2 Heri mtu yule ambaye Bwana
hamhesabii dhambi,
na ambaye rohoni mwake
hamna udanganyifu.
3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa
kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.
4 Usiku na mchana
mkono wako ulinilemea,
nguvu zangu zilinyonywa
kama vile katika joto la kiangazi.
5 Kisha nikakiri dhambi yangu kwako,
wala sikuficha uovu wangu.
Nilisema, “Nitaungama
makosa yangu kwa Bwana.”
Ndipo uliponisamehe
hatia ya dhambi yangu.
6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe
wakati unapopatikana,
hakika maji makuu yatakapofurika
hayatamfikia yeye.
7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,
utaniepusha na taabu
na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.
8 Nitakufundisha na kukuonesha njia utakayoiendea;
nitakushauri na kukuangalia.
9 Usiwe kama farasi au nyumbu
wasio na akili,
ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu
la sivyo hawatakukaribia.
10 Mtu mwovu ana taabu nyingi,
bali upendo usio na kikomo wa Bwana
unamzunguka mtu anayemtumaini.
11 Shangilieni katika Bwana na mfurahi, enyi wenye haki!
Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!
Currently Selected:
Zaburi 32: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.