Zaburi 28
28
Zaburi 28
Kuomba msaada
Zaburi ya Daudi.
1 Ninakuita wewe, Ee Bwana, Mwamba wangu;
usikatae kunisikiliza.
Kwa sababu ukinyamaza
nitafanana na walioshuka shimoni.
2 Sikia kilio changu nikikuomba unihurumie,
ninapokuita ili unisaidie,
ninapoinua mikono yangu kuelekea
Patakatifu pa Patakatifu pako.
3 Usiniburute pamoja na waovu,
pamoja na hao watendao mabaya,
ambao huzungumza na majirani zao maneno mazuri,
lakini mioyoni mwao wameficha chuki.
4 Walipe sawasawa na matendo yao,
sawasawa na matendo yao maovu;
walipe sawasawa na kazi za mikono yao,
uwalipe wanavyostahili.
5 Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Bwana,
na yale ambayo mikono yake imetenda,
atawabomoa na kamwe
hatawajenga tena.
6 Ahimidiwe Bwana,
kwa maana amesikia kilio changu
nikimwomba anihurumie.
7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu,
moyo wangu umemtumaini yeye,
nami nimesaidiwa.
Moyo wangu unarukaruka kwa furaha
nami nitamshukuru kwa wimbo.
8 Bwana ni nguvu ya watu wake,
ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.
9 Waokoe watu wako na uubariki urithi wako;
uwe mchungaji wao na uwabebe milele.
Currently Selected:
Zaburi 28: NEN
Highlight
Share
Compare
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.