Zaburi 103:13-22
Zaburi 103:13-22 NENO
Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo BWANA anavyowahurumia wale wanaomcha; kwa kuwa anajua tulivyoumbwa, anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi. Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani, anachanua kama ua la kondeni; upepo huvuma juu yake nalo hutoweka, mahali pake hapalikumbuki tena. Lakini kutoka milele hata milele upendo wa BWANA uko kwa wale wamchao, nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao: kwa wale walishikao agano lake na kukumbuka kuyatii mausia yake. BWANA ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni, na ufalme wake unatawala vitu vyote. Mhimidini BWANA, enyi malaika wake, ninyi mlio mashujaa, mnaozitii amri zake, ninyi mnaotii neno lake. Mhimidini BWANA, ninyi jeshi lake lote la mbinguni, ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake. Mhimidini BWANA, enyi kazi zake zote kila mahali katika milki yake.