Mithali 17
17
1 Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu
kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi.
2 Mtumishi mwenye hekima atamtawala mwana aaibishaye,
naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu.
3 Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu,
bali Bwana huujaribu moyo.
4Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya;
mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.
5 Yeye anaye mdhihaki maskini huonesha dharau kwa Muumba wake;
yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.
6 Wana wa wana ni taji la wazee,
nao wazazi ni fahari ya watoto wao.
7 Midomo yenye uwezo wa ushawishi
haimfai mpumbavu:
je, ni mibaya kiasi gani zaidi
midomo ya uongo kwa mtawala!
8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho;
kokote kigeukiapo, hufanikiwa.
9 Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo,
bali yeyote arudiaye jambo huwatenganisha rafiki wa karibu.
10Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua
kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.
11Mwovu hupenda kuasi tu;
mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake.
12 Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyangʼanywa watoto wake,
kuliko mpumbavu katika upumbavu wake.
13 Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema,
kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake.
14 Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji;
kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza.
15 Yeye asemaye kuwa asiye na haki ana haki,
naye asemaye kuwa mwenye haki hana haki:
Bwana huwachukia sana wote wawili.
16 Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu,
wakati yeye hana haja ya kupata hekima?
17 Rafiki hupenda wakati wote
naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.
18 Mtu mjinga huutoa mkono ili kuweka rehani,
naye huweka dhamana kwa jirani yake.
19Yeye apendaye ugomvi apenda dhambi;
naye ainuaye sana lango lake hutafuta uharibifu.
20Mtu mwenye moyo mpotovu hawezi kufanikiwa;
naye ambaye ulimi wake ni mdanganyifu huanguka kwenye taabu.
21 Kuwa na mwana mpumbavu huleta huzuni;
hakuna furaha kwa baba wa mpumbavu.
22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri,
bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.
23 Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri
ili kupotosha njia ya haki.
24 Mtu wa ufahamu huitazama hekima,
lakini macho ya mpumbavu huhangaika
hadi kwenye miisho ya dunia.
25 Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake
na uchungu kwa yeye aliyemzaa.
26 Si vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia,
au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao.
27 Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia,
naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu.
28 Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima akinyamaza,
na mwenye ufahamu akiuzuia ulimi wake.
Currently Selected:
Mithali 17: NEN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.