YouVersion Logo
Search Icon

Yohana 13

13
Yesu Awanawisha Wanafunzi Wake Miguu
1 Ilikuwa mara tu kabla ya Sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua ya kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni, naam, aliwapenda hadi kipimo cha mwisho.
2 Wakati alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni, wazo la kumsaliti Yesu. 3 Yesu akijua ya kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4 hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. 5 Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.
6 Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?”
7 Yesu akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.”
8 Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.”
Yesu akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.”
9Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!”
10 Yesu akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.” 11 Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi.
12Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.
18 “Sisemi hivi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni ili Andiko lipate kutimia, kwamba, ‘Yeye aliyekula chakula changu, ameinua kisigino chake dhidi yangu.’
19 “Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye. 20 Amin, amin nawaambia, yeyote anayempokea yule niliyemtuma anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.”
Yesu Anatabiri Kusalitiwa Kwake
(Mathayo 26:20-25; Marko 14:17-21; Luka 22:21-23)
21 Baada ya kusema haya, Yesu alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”
22Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. 23 Mmoja wa wanafunzi wake ambaye Yesu alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Yesu. 24Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.”
25 Yule mwanafunzi akamwegemea Yesu, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?”
26 Yesu akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. 27 Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia.
Yesu akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda litende haraka.” 28Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Yesu alimwambia hivyo. 29 Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Yesu alikuwa amemwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini chochote. 30 Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.
Yesu Atabiri Petro Kumkana
(Mathayo 26:31-35; Marko 14:27-31; Luka 22:31-34)
31 Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32 Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe naye atamtukuza mara.
33 “Watoto wangu, mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo. Mtanitafuta, na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, vivyo hivyo sasa nawaambia na ninyi. Niendako, ninyi hamwezi kuja.
34 “Amri mpya nawapa: Mpendane kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. 35 Kama mkipendana ninyi kwa ninyi, kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”
36 Simoni Petro akamuuliza, “Bwana, unakwenda wapi?”
Yesu akamjibu, “Ninakokwenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.”
37 Petro akamuuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako.”
38 Yesu akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin nakuambia, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

Currently Selected:

Yohana 13: NEN

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy