Waebrania 8
8
Kuhani Mkuu wa agano jipya
1 Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Aliye Mkuu mbinguni, 2yeye anayehudumu katika patakatifu, hema la kweli lililowekwa na Bwana, wala si na mwanadamu.
3 Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo, ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa. 4Kama angekuwa duniani, hangekuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria. 5Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Musa alionywa alipokaribia kujenga Maskani, akaambiwa: “Hakikisha kuwa unavitengeneza vitu vyote kwa mfano uliooneshwa kule mlimani.”#8:5 Kut 25:40 6Lakini huduma aliyopewa Yesu ni bora kuliko yao, kama vile agano ambalo yeye ni mpatanishi wake lilivyo bora zaidi ya lile la zamani, nalo limewekwa misingi ya ahadi zilizo bora zaidi.
7 Kwa maana kama hapakuwa na kasoro katika lile agano la kwanza, pasingekuwa na haja ya kutafuta nafasi kwa ajili ya jingine. 8Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema:
“Siku zinakuja, asema Bwana,
nitakapofanya agano jipya
na nyumba ya Israeli
na nyumba ya Yuda.
9 Agano langu halitakuwa kama lile
nililofanya na baba zao
nilipowashika mkono
kuwaongoza watoke nchi ya Misri,
kwa sababu hawakuendelea kuwa waaminifu katika agano langu,
nami nikawaacha, asema Bwana.
10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli
baada ya siku zile, asema Bwana.
Nitaziweka sheria zangu katika nia zao
na kuziandika mioyoni mwao.
Nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,
wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’
kwa sababu wote watanijua mimi,
tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.
12 Kwa sababu nitasamehe uovu wao,
wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”#8:12 Yer 31:31‑34
13 Kwa kuliita agano hili “jipya”, Mungu amefanya lile agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.
Currently Selected:
Waebrania 8: NEN
Highlight
Copy
Compare
Share
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.