Kutoka 15
15
Wimbo wa Musa na Miriamu
1 Ndipo Musa na Waisraeli wakamwimbia Bwana wimbo huu:
“Nitamwimbia Bwana,
kwa kuwa ametukuzwa sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.
2 “Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.
Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu,
Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
3 Bwana ni shujaa wa vita;
Bwana ndilo jina lake.
4 Magari ya vita ya Farao na jeshi lake
amewatosa baharini.
Maafisa wa Farao walio bora sana
wamezamishwa katika Bahari ya Shamu.
5 Maji yenye kina yamewafunika,
wamezama vilindini kama jiwe.
6 Mkono wako wa kuume, Ee Bwana
ulitukuka kwa uweza.
Mkono wako wa kuume, Ee Bwana,
ukamponda adui.
7 “Katika ukuu wa utukufu wako,
ukawaangusha chini wale waliokupinga.
Uliachia hasira yako kali,
ikawateketeza kama kapi.
8 Kwa pumzi ya pua yako
maji yalijilundika.
Mawimbi ya maji yakasimama imara kama ukuta,
vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari.
9 Adui alijivuna,
‘Nitawafuatia, nitawapata.
Nitagawanya nyara;
nitajishibisha kwao.
Nitafuta upanga wangu
na mkono wangu utawaangamiza.’
10 Lakini ulipuliza kwa pumzi yako,
bahari ikawafunika.
Wakazama kama risasi
kwenye maji makuu.
11 Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee Bwana?
Ni nani kama Wewe:
uliyetukuka katika utakatifu,
utishaye katika utukufu,
ukitenda maajabu?
12“Uliunyoosha mkono wako wa kuume
na nchi ikawameza.
13 Katika upendo wako usiokoma utawaongoza
watu uliowakomboa.
Katika nguvu zako utawaongoza
hadi makao yako matakatifu.
14 Mataifa watasikia na kutetemeka,
uchungu utawakamata Wafilisti.
15 Wakuu wa Edomu wataogopa,
viongozi wa Moabu watatetemeka kwa hofu,
Wakanaani watayeyuka,
16 vitisho na hofu vitawaangukia.
Kwa nguvu ya mkono wako
watatulia kama jiwe,
hadi watu wako wapite, Ee Bwana,
hadi watu uliowanunua wapite.
17 Utawaingiza na kuwapandikiza
juu ya mlima wa urithi wako:
hapo mahali, Ee Bwana,
ulipopafanya kuwa makao yako,
mahali patakatifu, Ee Bwana,
ulipopajenga kwa mikono yako.
18“Bwana atatawala
milele na milele.”
19 Farasi wa Farao, magari yake ya vita na wapanda farasi wake walipoingia baharini, Bwana aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika, lakini Waisraeli walipita baharini mahali pakavu. 20Kisha Miriamu yule nabii mke, ndugu yake Haruni, akachukua matari mkononi mwake na wanawake wote wakamfuata na matari yao wakicheza. 21Miriamu akawaimbia:
“Mwimbieni Bwana,
kwa maana ametukuka sana.
Farasi na mpanda farasi
amewatosa baharini.”
Maji ya Mara na Elimu
22Kisha Musa akawaongoza Israeli kutoka Bahari ya Shamu na kuingia katika Jangwa la Shuri. Kwa siku tatu walisafiri jangwani bila kupata maji. 23Walipofika Mara, hawakuweza kunywa maji yake kwa sababu yalikuwa machungu. (Ndiyo sababu mahali hapo panaitwa Mara#15:23 maana yake Chungu.) 24Kwa hiyo watu wakamnungʼunikia Musa, wakisema, “Tunywe nini?”
25 Ndipo Musa akamlilia Bwana, naye Bwana akamwonesha kipande cha mti. Akakitupa ndani ya maji, nayo maji yakawa matamu.
Huko Bwana akawapa amri na sheria na huko akawajaribu. 26Mungu akasema, “Mkisikiliza kwa makini sauti ya Bwana Mungu wenu na kuyafanya yaliyo mema machoni pake, na mkiyatii maagizo yake na kuzishika amri zake zote, sitaleta juu yenu ugonjwa wowote niliowaletea Wamisri, kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, niwaponyaye.”
27 Kisha wakafika Elimu, mahali palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na miti sabini ya mitende, wakapiga kambi huko karibu na maji.
Currently Selected:
Kutoka 15: NEN
Highlight
Copy
Compare
Share
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.