Zaburi 75:1-10
Zaburi 75:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Tunakushukuru, ee Mungu, tunakushukuru! Tunatangaza ukuu wa jina lako na kusimulia juu ya matendo yako makuu. Mungu asema: “Mimi nimeweka wakati maalumu! Wakati huo nitahukumu kwa haki. Nchi ikitetemeka na vyote vilivyomo, mimi ndiye ninayeitegemeza misingi yake. Nawaambia wenye kiburi: ‘Acheni kujigamba’; na waovu: ‘Msioteshe pembe za kiburi! Msijione kuwa watu wa maana sana, wala kusema maneno ya majivuno.’” Hukumu haitoki mashariki au magharibi; wala haitoki nyikani au mlimani. Mungu mwenyewe ndiye hakimu; humshusha mmoja na kumkweza mwingine. Mwenyezi-Mungu, anashika kikombe mkononi, kimejaa divai kali ya hasira yake; anaimimina na waovu wote wanainywa; naam, wanainywa mpaka tone la mwisho. Lakini mimi nitafurahi milele, nitamwimbia sifa Mungu wa Yakobo. Atavunja nguvu zote za watu waovu; lakini nguvu za waadilifu ataziimarisha.
Zaburi 75:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee Mungu, tunakushukuru. Tunakushukuru kwa kuwa Jina lako liko karibu; Watu huyasimulia matendo yako ya ajabu. Nitakapoufikia wakati ulioamriwa, Mimi nitahukumu hukumu za haki. Ingawa dunia na wote wakaao humo wataharuki, Mimi mwenyewe nimezisimamisha nguzo zake. Niliwaambia waliojivuna, Msijivune; Na wasio haki, Msiiinue pembe. Msiiinue pembe yenu juu, Wala msinene kwa shingo ya kiburi. Maana siko mashariki wala magharibi, Wala nyikani itokako heshima. Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili huyu na kumwinua huyu. Maana mkononi mwa BWANA mna kikombe, Na mvinyo yake inatoka povu; Kumejaa machanganyiko; Naye huyamimina. Na sira zake wasio haki wa dunia Watazifyonza na kuzinywa. Bali mimi nitatangaza matendo yako milele, Nitamwimbia Mungu wa Yakobo. Nguvu zote za wasio haki nitazimaliza, Lakini nguvu za mwenye haki nitaziimarisha.
Zaburi 75:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee Mungu, twakushukuru. Twakushukuru kwa kuwa Jina lako li karibu; Watu huyasimulia matendo yako ya ajabu. Nitakapoufikia wakati ulioamriwa, Mimi nitahukumu hukumu za haki. Ingawa dunia na wote wakaao humo wataharuki, Mimi mwenyewe nimezisimamisha nguzo zake. Naliwaambia waliojivuna, Msijivune; Na wasio haki, Msiiinue pembe. Msiiinue pembe yenu juu, Wala msinene kwa shingo ya kiburi. Maana siko mashariki wala magharibi, Wala nyikani itokako heshima. Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili huyu na kumwinua huyu. Maana mkononi mwa BWANA mna kikombe, Na mvinyo yake inatoka povu; Kumejaa machanganyiko; Naye huyamimina. Na sira zake wasio haki wa dunia Watazifyonza na kuzinywa. Bali mimi nitatangaza matendo yako milele, Nitamwimbia Mungu wa Yakobo. Pembe zote za wasio haki nitazikata, Na pembe za mwenye haki zitainuka.
Zaburi 75:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ee Mungu, tunakushukuru, tunakushukuru wewe, kwa kuwa jina lako li karibu; watu husimulia matendo yako ya ajabu. Unasema, “Ninachagua wakati maalum; ni mimi nihukumuye kwa haki. Wakati dunia na watu wake wote inapotetemeka, ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara. Kwa wale wenye majivuno ninasema, ‘Msijisifu tena,’ kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu. Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu; msiseme kwa shingo zilizonyooshwa.’ ” Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu. Bali Mungu ndiye ahukumuye: Humshusha huyu na kumkweza mwingine. Mkononi mwa BWANA kuna kikombe kilichojaa mvinyo unaotoka povu uliochanganywa na vikolezo; huumimina, nao waovu wote wa dunia hunywa mpaka tone la mwisho. Bali mimi, nitatangaza hili milele; nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo. Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote, bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu.