Zaburi 111:1-10
Zaburi 111:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Nitamshukuru Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote, nikijumuika na jamii ya watu waadilifu. Matendo ya Mwenyezi-Mungu ni makuu mno! Wote wanaoyafurahia huyatafakari. Kila afanyacho kimejaa utukufu na fahari; uadilifu wake wadumu milele. Amesababisha matendo yake ya ajabu yakumbukwe; Mwenyezi-Mungu ni mwema na mwenye huruma. Huwapa chakula wenye kumcha; hasahau kamwe agano lake. Amewaonesha watu wake nguvu ya matendo yake, amewapa nchi za mataifa mengine ziwe mali yao. Matendo yake ni ya haki na ya kuaminika; kanuni zake zote ni za kutegemewa. Amri zake zadumu daima na milele; zimetolewa kwa haki na uadilifu. Aliwakomboa watu wake na kufanya nao agano la milele. Yeye ni mtakatifu na wa kutisha mno! Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima; wote wanaozitii amri zake hujaliwa busara. Sifa zake zadumu milele.
Zaburi 111:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haleluya. Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote, Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano. Matendo ya BWANA ni makuu, Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo. Kazi yake imejaa heshima na adhama, Na haki yake yadumu milele. Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu; BWANA ni mwenye fadhili na rehema. Amewapa wamchao chakula; Atalikumbuka agano lake milele. Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake, Kwa kuwapa urithi wa mataifa. Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu, Maagizo yake yote ni amini, Yamethibitika milele na milele, Yamefanywa kwa uaminifu na haki. Amewapelekea watu wake ukombozi, Ameamuru agano lake liwe la milele, Jina lake ni takatifu na la kuogopwa. Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana ufahamu mzuri, Sifa zake zadumu milele.
Zaburi 111:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haleluya. Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote, Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano. Matendo ya BWANA ni makuu, Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo. Kazi yake ni heshima na adhama, Na haki yake yakaa milele. Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu; BWANA ni mwenye fadhili na rehema. Amewapa wamchao chakula; Atalikumbuka agano lake milele. Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake, Kwa kuwapa urithi wa mataifa. Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu, Maagizo yake yote ni amini, Yamethibitika milele na milele, Yamefanywa katika kweli na adili. Amewapelekea watu wake ukombozi, Ameamuru agano lake liwe la milele, Jina lake ni takatifu la kuogopwa. Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele.
Zaburi 111:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Msifuni BWANA. Nitamtukuza BWANA kwa moyo wangu wote, katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko. Kazi za BWANA ni kuu, wote wanaopendezwa nazo huzitafakari. Kazi zake zimejaa fahari na utukufu, haki yake hudumu daima. Amefanya maajabu yake yakumbukwe, BWANA ni mwenye neema na huruma. Huwapa chakula wale wanaomcha, hulikumbuka agano lake milele. Amewaonesha watu wake uwezo wa kazi zake, akiwapa nchi za mataifa mengine. Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki, mausia yake yote ni ya kuaminika. Zinadumu milele na milele, zikifanyika kwa uaminifu na unyofu. Aliwapa watu wake ukombozi, aliamuru agano lake milele: jina lake ni takatifu na la kuogopwa. Kumcha BWANA ndicho chanzo cha hekima, wote wanaozifuata amri zake wana busara. Sifa zake zadumu milele.