Methali 4:6-24
Methali 4:6-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Usimwache Hekima, naye atakutunza; umpende, naye atakulinda. Jambo la msingi ni kujipatia hekima; toa vyote ulivyonavyo ujipatie akili. Mthamini sana Hekima, naye atakutukuza; ukimshikilia atakupa heshima. Atakuvika kilemba kizuri kichwani pako, atakupa taji maridadi.” Mwanangu, sikia na kuyapokea maneno yangu, ili upate kuwa na miaka mingi ya kuishi. Nimekufundisha njia ya hekima, nimekuongoza katika njia nyofu. Ukitembea hatua zako hazitazuiwa, wala ukikimbia hutajikwaa. Zingatia mafundisho ya Hekima na usimwache aponyoke, mshike kwa makini maana yeye ni uhai wako. Usijiingize katika njia ya waovu, wala usifuate mwenendo wa watu wabaya. Iepe njia hiyo wala usiikaribie; jiepushe nayo, uende zako. Waovu kamwe hawalali wasipotenda uovu; hawapati usingizi wasipomkwaza mtu. Maana uovu ndicho chakula chao, ukatili ndiyo divai yao. Njia ya watu wema ni kama nuru ya alfajiri, ambayo hungaa zaidi na zaidi hata mchana kamili. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene, hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, sikiliza kwa makini maneno yangu, itegee sikio misemo yangu. Usiyaache yatoweke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako. Maana hayo ni uhai kwa mtu anayeyapata, ni dawa kwa mwili wake wote. Linda moyo wako kwa uangalifu wote, maana humo zatoka chemchemi za uhai. Tenga mbali nawe lugha potovu; wala midomo yako isitamke maneno madanganyifu.
Methali 4:6-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usimwache, naye atakusitiri; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia. Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji la uzuri. Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu. Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako. Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya ujeuri. Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing'aayo, Ikizidi kung'aa hata mchana mkamilifu. Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho. Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Jiepushe na kinywa cha ujeuri, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.
Methali 4:6-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia. Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji ya uzuri. Mwanangu, sikiliza, na kuzipokea kauli zangu; Na miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Nimekufundisha katika njia ya hekima; Nimekuongoza katika mapito ya unyofu. Uendapo, hatua zako hazitadhiikika, Wala ukipiga mbio hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako. Usiingie katika njia ya waovu, Wala usitembee katika njia ya wabaya. Jiepushe nayo, usipite karibu nayo, Igeukie mbali, ukaende zako. Maana hawalali isipokuwa wametenda madhara; Huondolewa usingizi, ikiwa hawakumwangusha mtu. Maana wao hula mkate wa uovu, Nao hunywa divai ya jeuri. Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, Ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu. Njia ya waovu ni kama giza; Hawajui ni kitu gani kiwakwazacho. Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote. Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Kinywa cha ukaidi ukitenge nawe, Na midomo ya upotovu uiweke mbali nawe.
Methali 4:6-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Usimwache hekima naye atakuweka salama; mpende, naye atakulinda. Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu. Mstahi, naye atakukweza; mkumbatie, naye atakuheshimu. Atakuvika shada la neema kichwani mwako na kukupa taji la utukufu.” Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi. Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito ya unyoofu. Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa; ukimbiapo, hutajikwaa. Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako. Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu, wala usitembee katika njia ya wapotovu. Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo; achana nayo, na uelekee njia yako. Kwa kuwa hawawezi kulala hadi watende uovu; wanashindwa hata kusinzia hadi wamwangushe mtu. Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri. Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, ambayo hungʼaa zaidi na zaidi hadi mchana mkamilifu. Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; hawajui kinachowafanya wajikwae. Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia; sikiliza kwa makini maneno yangu. Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako; kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu. Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.