Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13:24-58

Mathayo 13:24-58 Biblia Habari Njema (BHN)

Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja, akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake. Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana. Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, ‘Bwana, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?’ Yeye akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya hivyo’. Basi, watumishi wake wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayangoe?’ Naye akawajibu, ‘La, msije labda mnapokusanya magugu, mkangoa na ngano pia. Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: Kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.’” Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake. Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikisha ota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.” Yesu akawaambia mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga madebe mawili na nusu, hata unga wote ukaumuka.” Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano, ili jambo lililonenwa na nabii litimie: “Nitasema nao kwa mifano; nitafichua yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu.” Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani.” Yesu akawaambia, “Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu. Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu. Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika. Kama vile magugu yanavyokusanywa na kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati; Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu, na kuwatupa katika tanuri ya moto, na huko watalia na kusaga meno. Kisha, wale wema watangara kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie! “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri. Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina. Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: Malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema, na kuwatupa hao wabaya katika tanuri ya moto. Huko watalia na kusaga meno.” Yesu akawauliza, “Je, mmeelewa mambo haya yote?” Wakamjibu, “Naam.” Naye akawaambia, “Hivyo basi, kila mwalimu wa sheria anayekuwa mwanafunzi wa ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.” Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo, akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi lao hata wakashangaa, wakasema, “Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu? Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi, amepata wapi haya yote?” Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!” Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.

Shirikisha
Soma Mathayo 13

Mathayo 13:24-58 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika shamba lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hadi wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko miboga yote ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kukaa katika matawi yake. Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia katika nyumba; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya shambani. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile shamba ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuri ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuri ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika mji wa kwao, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na dada zake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutoamini kwao.

Shirikisha
Soma Mathayo 13

Mathayo 13:24-58 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake. Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali. Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Shirikisha
Soma Mathayo 13

Mathayo 13:24-58 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea. “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’ “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’ “Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayangʼoe?’ “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyangʼoe, kwa maana wakati mkingʼoa magugu mnaweza mkangʼoa na ngano pamoja nayo. Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja hadi wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ” Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake. Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.” Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga hadi wote ukaumuka.” Yesu alinena mambo haya yote kwa umati wa watu kwa mifano, wala hakuwaambia lolote pasipo mfano. Hii ilikuwa ili kutimiza neno lililonenwa na nabii, aliposema: “Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano; nitahubiri mambo yaliyofichika tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.” Kisha Yesu akaagana na ule umati, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.” Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika. “Kama vile magugu yangʼolewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watangʼaa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie. “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua. “Tena, ufalme wa mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. Ulipojaa, wavuvi wakauvuta ufuoni, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.” Yesu akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?” Wakamjibu, “Ndiyo.” Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliyefundishwa elimu ya ufalme wa mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.” Yesu alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka. Alipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza? Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Mariamu, nao ndugu zake si Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? Nao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?” Wakachukizwa naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake.” Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Shirikisha
Soma Mathayo 13