Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mt 13

13
Mfano wa Mpanzi
1 # Mk 4:1-20; Lk 8:4-15 Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. 2#Lk 5:1-3Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. 3Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. 4Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; 5nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; 6na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. 7Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; 8nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. 9Mwenye masikio na asikie.
Sababu ya kusema kwa Mifano
10Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? 11Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. 12#Mt 25:29; Mk 4:25; Lk 8:18; 19:26Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. 13#Kum 29:4Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. 14#Isa 6:9-10; Yn 12:40; Mdo 28:26,27Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema,
Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa;
Kutazama mtatazama, wala hamtaona.
15Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito,
Na kwa masikio yao hawasikii vema,
Na macho yao wameyafumba;
Wasije wakaona kwa macho yao,
Wakasikia kwa masikio yao,
Wakaelewa kwa mioyo yao,
Wakaongoka, nikawaponya.
16 # Lk 10:23-24 Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. 17Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.
Maelezo ya Mfano wa Mpanzi
18Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. 19Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia. 20Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; 21lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa. 22#Mt 6:19-34; 1 Tim 6:9Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. 23Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.
Mfano wa Magugu katikati ya Ngano
24 # Mt 13:36-43 Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; 25lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. 26Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. 27Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? 28Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? 29Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. 30#Mt 3:12Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.
Mfano wa Punje ya Haradali
31 # Mk 4:30-32; Lk 13:18,19 Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; 32#Dan 4:12,21; Eze 17:23; 31:6; Zab 104:12nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.
Mfano wa Chachu
33 # Lk 13:20,21 Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.
Matumizi ya Mifano
34 # Mk 4:33,34 Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; 35#Zab 78:2ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,
Nitafumbua kinywa changu kwa mifano,
Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.
Yesu aelezea Mfano wa Magugu
36 # Mt 13:24-30 Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni. 37Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; 38#1 Kor 3:9lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; 39yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. 40#Yn 15:6Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. 41#Sef 1:3; Mt 25:31-46; 7:23Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, 42#Mt 8:12na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. 43#Dan 12:3Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.
Mifano Mitatu
44 # Mt 19:29; Lk 14:33; Flp 3:7; Mit 2:4 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile.
45Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; 46#Mit 8:10,11naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.
47 # Mt 22:9,10 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna; 48hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. 49#Mt 25:32Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, 50na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Hazina Mpya na ya Kale
51Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. 52Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.
53 # Mk 6:1-6; Lk 4:15-30 Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.
Kukataliwa kwa Yesu katika Nazareti
54 # Mt 7:28; 11:1; 19:1; 26:1 Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? 55Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? 56#Yn 7:15,52Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? 57#Yn 4:44Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. 58Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Iliyochaguliwa sasa

Mt 13: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha