Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13:24-58

Mathayo 13:24-58 SRUV

Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika shamba lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika shamba lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hadi wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu. Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko miboga yote ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kukaa katika matawi yake. Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia katika nyumba; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya shambani. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile shamba ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika wake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuri ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuri ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika mji wa kwao, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na dada zake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutoamini kwao.

Soma Mathayo 13