Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 21:1-19

Yoshua 21:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Walipokuwa huko Shilo katika nchi ya Kanaani viongozi wa koo za Walawi wakawaendea kuhani Eleazari na Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa za makabila yote ya Waisraeli, wakawaambia, “Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose tupewe miji ya kuishi na mbuga za malisho ya wanyama wetu.” Basi, kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu, Waisraeli walichagua kutoka katika maeneo ya nchi zao, miji na vijiji vya malisho, wakawapa Walawi iwe sehemu yao. Kura ya kwanza ilizipata jamaa za ukoo wa Kohathi. Miongoni mwao wazawa wa kuhani Aroni walipewa kwa kura, miji iliyokuwa katika maeneo ya makabila ya Yuda, Simeoni, na Benyamini. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na mitatu. Watu wa ukoo wa Kohathi waliosalia walipewa miji kumi iliyoko katika maeneo ya makabila ya Efraimu, Dani na katika eneo la nusu ya kabila la Manase. Watu wa ukoo wa Gershoni walipewa kwa kura miji kumi na mitatu katika maeneo ya makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na katika eneo la nusu ya kabila la Manase huko Bashani. Jamaa za ukoo wa Merari walipewa miji kumi na miwili katika maeneo ya makabila ya Reubeni, Gadi na Zebuluni. Waisraeli waliwapa Walawi miji hiyo pamoja na vijiji vya malisho yao, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza Mose. Yafuatayo ni majina ya miji kutoka kwenye maeneo ya kabila la Yuda na Simeoni ambayo ilitolewa kwa wazawa wa kuhani Aroni, waliokuwa jamaa za ukoo wa Kohathi ambaye alikuwa wa kabila la Lawi. Sehemu yao walipata kwanza kwani kura yao ilitokea kwanza. Walipewa Kiriath-arba yaani Hebroni (Arba alikuwa baba yake Anaki) katika milima ya Yuda, pamoja na mbuga zilizoizunguka. Lakini mashamba ya mji huo pamoja na vijiji vilivyouzunguka alikuwa amekwisha pewa Kalebu mwana wa Yefune viwe mali yake. Licha ya kuwapa wazawa wa kuhani Aroni mji wa Hebroni ambao pia ulikuwa umetengwa kuwa mji wa kukimbilia usalama, waliwapa miji ya Libna pamoja na mbuga zake za malisho, Yatiri pamoja na mbuga zake za malisho, Eshtemoa pamoja na mbuga zake za malisho, Holoni pamoja na mbuga zake za malisho, Debiri pamoja na mbuga zake za malisho, Aini pamoja na mbuga zake za malisho, Yuta pamoja na mbuga zake za malisho na Beth-shemeshi pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji hiyo iliyo katika maeneo ya makabila hayo mawili ni tisa. Katika eneo la kabila la Benyamini walipewa miji mingine: Gibeoni pamoja na mbuga zake za malisho, Anathothi pamoja na mbuga zake za malisho, Almoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. Miji yote ya wazawa wa Aroni ambao walikuwa makuhani, ilikuwa kumi na mitatu pamoja na mbuga zao za malisho.

Shirikisha
Soma Yoshua 21

Yoshua 21:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakati huo hao vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi wakamwendea kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni na viongozi wa hao waliokuwa viongozi wa familia za makabila ya Waisraeli; wakanena nao hapo Shilo katika nchi ya Kanaani, wakisema, Yeye BWANA aliamuru kwa mkono wa Musa kwamba sisi tupewe miji tupate kukaa humo, mbuga zake za malisho kwa ajili ya mifugo wetu. Basi wana wa Israeli wakawapa Walawi miji hii, pamoja na mbuga zake za malisho, katika urithi wao, sawasawa na hiyo amri ya BWANA. Kura ikatokea kwa ajili ya jamaa za Wakohathi; na wana wa Haruni kuhani, waliokuwa katika Walawi, walipata miji kumi na mitatu kwa kura katika kabila la Yuda, na katika kabila la Simeoni, na katika kabila la Benyamini. Kisha Wakohathi wengine waliosalia walipata kwa kura miji kumi katika jamaa za kabila la Efraimu, na katika kabila la Dani, na katika hiyo nusu ya kabila la Manase. Tena wana wa Gershoni walipata kwa kura miji kumi na mitatu katika jamaa za kabila la Isakari, na katika kabila la Asheri, na katika kabila la Naftali, na katika hiyo nusu ya kabila la Manase huko Bashani. Na wana wa Merari kwa kufuata jamaa zao walipata miji kumi na miwili katika kabila la Reubeni, na katika kabila la Gadi, na katika kabila la Zabuloni. Kisha wana wa Israeli waliwapa Walawi kwa kura miji hiyo pamoja na mbuga zake za malisho, kama BWANA alivyoamuru kwa mkono wa Musa. Kisha wakawapa katika kabila la wana wa Yuda, na katika kabila la wana wa Simeoni, miji hii iliyotajwa hapa kwa majina; nayo ilikuwa kwa ajili ya wana wa Haruni, wa jamaa ya Wakohathi, waliokuwa wa wana wa Lawi; kwa kuwa kura ya kwanza ilikuwa ni yao. Nao wakawapa Kiriath-arba, ndio Hebroni, (huyo Arba alikuwa baba yake Anaki), katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na mbuga zake za malisho yaliyouzunguka pande zote. Lakini mashamba ya mji, na vile vijiji vyake, wakampa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake. Kisha wakawapa wana wa Haruni, kuhani, Hebroni pamoja na mbuga zake za malisho yake, huo mji wa kukimbilia kwa ajili ya mwuaji, na Libna pamoja na malisho yake; na Yatiri pamoja na mbuga zake za malisho, na Eshtemoa pamoja na mbuga zake za malisho; na Holoni pamoja na mbuga zake za malisho, na Debiri pamoja na mbuga zake za malisho; na Aini, pamoja na mbuga zake za malisho, na Yuta pamoja na mbuga zake za malisho, na Beth-shemeshi pamoja na mbuga zake za malisho; miji tisa katika makabila hayo mawili. Tena katika kabila la Benyamini, Gibeoni pamoja na mbuga zake za malisho, na Geba pamoja na mbuga zake za malisho; na Anathothi pamoja na mbuga zake za malisho, na Almoni pamoja na mbuga zake za malisho; miji minne. Miji yote ya wana wa Haruni, makuhani, ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na mbuga zake za malisho.

Shirikisha
Soma Yoshua 21

Yoshua 21:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wakati huo hao vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi wakamwendea Eleazari, kuhani, na Yoshua, mwana wa Nuni, na hao waliokuwa vichwa vya nyumba za mababa ya kabila za wana wa Israeli; wakanena nao hapo Shilo katika nchi ya Kanaani, wakisema, Yeye BWANA aliamuru kwa mkono wa Musa kwamba sisi tupewe miji tupate kukaa humo, pamoja na malisho yake kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo. Basi wana wa Israeli wakawapa Walawi miji hii, pamoja na malisho yake, katika urithi wao, sawasawa na hiyo amri ya BWANA. Kura ikatokea kwa ajili ya jamaa za Wakohathi; na wana wa Haruni kuhani, waliokuwa katika Walawi, walipata miji kumi na mitatu kwa kura katika kabila ya Yuda, na katika kabila ya Simeoni, na katika kabila ya Benyamini. Kisha Wakohathi wengine waliosalia walipata kwa kura katika jamaa za kabila ya Efraimu, na katika kabila ya Dani, na katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, miji kumi. Tena wana wa Gershoni walipata kwa kura katika jamaa za kabila ya Isakari, na katika kabila ya Asheri, na katika kabila ya Naftali, na katika hiyo nusu ya kabila ya Manase huko Bashani, miji kumi na mitatu. Na wana wa Merari kwa kuandama jamaa zao walipata katika kabila ya Reubeni, na katika kabila ya Gadi, na katika kabila ya Zabuloni, miji kumi na miwili. Kisha wana wa Israeli waliwapa Walawi kwa kura miji hiyo pamoja na malisho yake, kama BWANA alivyoamuru kwa mkono wa Musa. Kisha wakawapa katika kabila ya wana wa Yuda, na katika kabila ya wana wa Simeoni, miji hii iliyotajwa hapa kwa majina; nayo ilikuwa kwa ajili ya wana wa Haruni, wa jamaa ya Wakohathi, waliokuwa wa wana wa Lawi; kwa kuwa kura ya kwanza ilikuwa ni yao. Nao wakawapa Kiriath-arba, huyo Arba alikuwa baba yake Anaki, (ndio Hebroni), katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na malisho yake yaliyouzunguka pande zote. Lakini mashamba ya mji, na vile vijiji vyake, wakampa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake. Kisha wakawapa wana wa Haruni kuhani Hebroni pamoja na malisho yake, huo mji wa kukimbilia kwa ajili ya mwuaji, na Libna pamoja na malisho yake; na Yatiri pamoja na malisho yake, na Eshtemoa pamoja na malisho yake; na Holoni pamoja na malisho yake, na Debiri pamoja na malisho yake; na Aini pamoja na malisho yake, na Yuta pamoja na malisho yake, na Bethshemeshi pamoja na malisho yake; miji kenda katika kabila hizo mbili. Tena katika kabila ya Benyamini, Gibeoni pamoja na malisho yake, na Geba pamoja na malisho yake; na Anathothi pamoja na malisho yake, na Almoni pamoja na malisho yake; miji minne. Miji yote ya wana wa Haruni, makuhani, ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na malisho yake.

Shirikisha
Soma Yoshua 21

Yoshua 21:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi viongozi wa jamaa ya Walawi, wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa nyingine za makabila ya Israeli huko Shilo katika Kanaani na kuwaambia, “BWANA aliamuru kupitia Musa kuwa mtupe miji ya kuishi yenye maeneo ya malisho kwa mifugo yetu.” Hivyo kama vile BWANA alivyoamuru, Waisraeli wakawapa Walawi miji ifuatayo, na maeneo ya malisho ya kila mji kutoka urithi wao wenyewe. Kura ya kwanza ikaangukia Wakohathi, kufuatana na koo zao. Walawi waliokuwa wazao wa kuhani Haruni walipewa miji kumi na tatu kutoka makabila ya Yuda, Simeoni na Benyamini. Wazao wengine waliobaki wa Wakohathi walipewa miji kumi kutoka koo za makabila ya Efraimu, Dani na nusu ya Manase. Wazao wa Gershoni walipewa miji kumi na tatu kutoka koo za makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na nusu ya Manase huko Bashani. Wazao wa Merari, kufuatana na koo zao, walipewa miji kumi na mbili kutoka makabila ya Reubeni, Gadi na Zabuloni. Kwa hiyo Waisraeli wakawapa Walawi miji hii na maeneo ya malisho ya kila mji, kama BWANA alivyoamuru kupitia kwa Musa. Kutoka makabila ya Yuda na Simeoni waligawa miji ifuatayo kwa majina (miji hii walipewa wazao wa Haruni ambao walitokana na koo za Wakohathi wa Walawi, kwa sababu kura ya kwanza iliwaangukia): Waliwapa Kiriath-Arba (yaani Hebroni), pamoja na eneo lake la malisho lililouzunguka, katika nchi ya vilima ya Yuda. (Arba alikuwa baba wa Anaki.) Lakini mashamba na vijiji vilivyouzunguka mji walikuwa wamempa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake. Kwa hiyo wazao wa kuhani Haruni wakapewa Hebroni (mji mkuu wa makimbilio kwa ajili ya yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji), Libna, Yatiri, Eshtemoa, Holoni, Debiri, Aini, Yuta na Beth-Shemeshi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji tisa kutoka kwa makabila haya mawili. Kutoka kabila la Benyamini wakawapa Gibeoni, Geba, Anathothi na Almoni, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne. Miji yote waliyopewa makuhani, wazao wa Haruni, ilikuwa kumi na tatu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.

Shirikisha
Soma Yoshua 21