Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 21:1-19

Yoshua 21:1-19 NENO

Basi viongozi wa jamaa ya Walawi, wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa nyingine za makabila ya Israeli huko Shilo katika Kanaani na kuwaambia, “BWANA aliamuru kupitia Musa kuwa mtupe miji ya kuishi yenye maeneo ya malisho kwa mifugo yetu.” Hivyo kama vile BWANA alivyoamuru, Waisraeli wakawapa Walawi miji ifuatayo, na maeneo ya malisho ya kila mji kutoka urithi wao wenyewe. Kura ya kwanza ikaangukia Wakohathi, kufuatana na koo zao. Walawi waliokuwa wazao wa kuhani Haruni walipewa miji kumi na tatu kutoka makabila ya Yuda, Simeoni na Benyamini. Wazao wengine waliobaki wa Wakohathi walipewa miji kumi kutoka koo za makabila ya Efraimu, Dani na nusu ya Manase. Wazao wa Gershoni walipewa miji kumi na tatu kutoka koo za makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na nusu ya Manase huko Bashani. Wazao wa Merari, kufuatana na koo zao, walipewa miji kumi na mbili kutoka makabila ya Reubeni, Gadi na Zabuloni. Kwa hiyo Waisraeli wakawapa Walawi miji hii na maeneo ya malisho ya kila mji, kama BWANA alivyoamuru kupitia kwa Musa. Kutoka makabila ya Yuda na Simeoni waligawa miji ifuatayo kwa majina (miji hii walipewa wazao wa Haruni ambao walitokana na koo za Wakohathi wa Walawi, kwa sababu kura ya kwanza iliwaangukia): Waliwapa Kiriath-Arba (yaani Hebroni), pamoja na eneo lake la malisho lililouzunguka, katika nchi ya vilima ya Yuda. (Arba alikuwa baba wa Anaki.) Lakini mashamba na vijiji vilivyouzunguka mji walikuwa wamempa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake. Kwa hiyo wazao wa kuhani Haruni wakapewa Hebroni (mji mkuu wa makimbilio kwa ajili ya yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji), Libna, Yatiri, Eshtemoa, Holoni, Debiri, Aini, Yuta na Beth-Shemeshi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji tisa kutoka kwa makabila haya mawili. Kutoka kabila la Benyamini wakawapa Gibeoni, Geba, Anathothi na Almoni, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne. Miji yote waliyopewa makuhani, wazao wa Haruni, ilikuwa kumi na tatu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.