Yoshua 21:1-19
Yoshua 21:1-19 SRUV
Wakati huo hao vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi wakamwendea kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni na viongozi wa hao waliokuwa viongozi wa familia za makabila ya Waisraeli; wakanena nao hapo Shilo katika nchi ya Kanaani, wakisema, Yeye BWANA aliamuru kwa mkono wa Musa kwamba sisi tupewe miji tupate kukaa humo, mbuga zake za malisho kwa ajili ya mifugo wetu. Basi wana wa Israeli wakawapa Walawi miji hii, pamoja na mbuga zake za malisho, katika urithi wao, sawasawa na hiyo amri ya BWANA. Kura ikatokea kwa ajili ya jamaa za Wakohathi; na wana wa Haruni kuhani, waliokuwa katika Walawi, walipata miji kumi na mitatu kwa kura katika kabila la Yuda, na katika kabila la Simeoni, na katika kabila la Benyamini. Kisha Wakohathi wengine waliosalia walipata kwa kura miji kumi katika jamaa za kabila la Efraimu, na katika kabila la Dani, na katika hiyo nusu ya kabila la Manase. Tena wana wa Gershoni walipata kwa kura miji kumi na mitatu katika jamaa za kabila la Isakari, na katika kabila la Asheri, na katika kabila la Naftali, na katika hiyo nusu ya kabila la Manase huko Bashani. Na wana wa Merari kwa kufuata jamaa zao walipata miji kumi na miwili katika kabila la Reubeni, na katika kabila la Gadi, na katika kabila la Zabuloni. Kisha wana wa Israeli waliwapa Walawi kwa kura miji hiyo pamoja na mbuga zake za malisho, kama BWANA alivyoamuru kwa mkono wa Musa. Kisha wakawapa katika kabila la wana wa Yuda, na katika kabila la wana wa Simeoni, miji hii iliyotajwa hapa kwa majina; nayo ilikuwa kwa ajili ya wana wa Haruni, wa jamaa ya Wakohathi, waliokuwa wa wana wa Lawi; kwa kuwa kura ya kwanza ilikuwa ni yao. Nao wakawapa Kiriath-arba, ndio Hebroni, (huyo Arba alikuwa baba yake Anaki), katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na mbuga zake za malisho yaliyouzunguka pande zote. Lakini mashamba ya mji, na vile vijiji vyake, wakampa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake. Kisha wakawapa wana wa Haruni, kuhani, Hebroni pamoja na mbuga zake za malisho yake, huo mji wa kukimbilia kwa ajili ya mwuaji, na Libna pamoja na malisho yake; na Yatiri pamoja na mbuga zake za malisho, na Eshtemoa pamoja na mbuga zake za malisho; na Holoni pamoja na mbuga zake za malisho, na Debiri pamoja na mbuga zake za malisho; na Aini, pamoja na mbuga zake za malisho, na Yuta pamoja na mbuga zake za malisho, na Beth-shemeshi pamoja na mbuga zake za malisho; miji tisa katika makabila hayo mawili. Tena katika kabila la Benyamini, Gibeoni pamoja na mbuga zake za malisho, na Geba pamoja na mbuga zake za malisho; na Anathothi pamoja na mbuga zake za malisho, na Almoni pamoja na mbuga zake za malisho; miji minne. Miji yote ya wana wa Haruni, makuhani, ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na mbuga zake za malisho.