Yobu 36:1-25
Yobu 36:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Elihu akaendelea kusema: “Nivumilie kidogo, nami nitakuonesha kitu; maana bado ninacho cha kusema kwa niaba ya Mungu. Nitaleta hekima yangu kutoka mbali sana, na kuonesha kwamba Muumba wangu ni mwadilifu. Kweli maneno yangu si ya uongo; mwenye elimu kamili yuko hapa nawe. “Sikiliza Mungu ni mwenye nguvu wala hamdharau mtu yeyote; uwezo wa akili yake ni mkuu mno! Hawaachi waovu waendelee kuishi; lakini huwapatia wanaodhulumiwa haki zao. Haachi kuwalinda watu waadilifu; huwatawaza, wakatawala na kutukuka. Lakini kama watu wamefungwa minyororo, wamenaswa katika kamba za mateso, Mungu huwaonesha matendo yao maovu, na kwamba wao ni watu wenye kiburi. Huwafungua masikio wasikie mafunzo, na kuwaamuru warudi na kuacha uovu. Wakimtii Mungu na kumtumikia, hufanikiwa katika siku zao zote; miaka yao yote huwa ya furaha. Lakini wasipomtii, huangamia kwa upanga, na kufa kwa kukosa akili. “Wasiomcha Mungu hupenda kukasirika, hawamlilii msaada anapowabana. Hufa wangali bado vijana, maisha yao huisha kama ya walawiti. Lakini Mungu huwaokoa wanyonge kwa unyonge wao hutumia shida zao kuwafumbua macho. Mungu alikuvuta akakutoa taabuni, akakuweka mahali pa wasaa pasipo shida, na mezani pako akakuandalia vinono. “Lakini sasa umehukumiwa kama mwovu, hukumu ya haki imekukumba. Jihadhari ghadhabu isije ikakufanya ukadhihaki, au ukubwa wa mali za kukukomboa ukakupotosha. Je, kilio chako kitafaa kukutoa taabuni, au nguvu zako zote zitakusaidia? Usitamani usiku uje, ambapo watu hufanywa watoweke walipo. Jihadhari! Usiuelekee uovu maana umepatiwa mateso kukuepusha na uovu. Kumbuka ukuu wa uwezo wa Mungu; nani awezaye kumfundisha kitu? Nani basi aliyeweza kumpangia njia yake, au awezaye kumwambia: ‘Umekosea?’ “Usisahau kuyasifu matendo yake; ambayo watu wameyashangilia. Watu wote wameona aliyofanya Mungu; binadamu huyaona kutoka mbali.
Yobu 36:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena Elihu akaendelea na kusema, Ningojee kidogo nami nitakueleza; Kwa kuwa ningali na maneno kwa ajili ya Mungu. Nitayaleta maarifa yangu kutoka mbali, Nami nitampa haki Muumba wangu. Maana hakika maneno yangu si ya uongo; Aliyekamilika katika maarifa yu pamoja nawe. Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu yeyote; Ana uweza katika nguvu za fahamu. Hauhifadhi uhai wa waovu; Lakini huwapa wateswao haki yao. Yeye hawaondolei macho yake wenye haki; Lakini pamoja na wafalme huwaweka Katika viti vya enzi milele, nao hutukuzwa. Nao wakifungwa kwa pingu, Wakitwaliwa kwa kamba za mateso; Ndipo huwaonesha matendo yao, Na makosa yao, ya kuwa wametenda kwa kujivuna. Yeye huyafunua masikio yao, wasikie maonyo, Na kuwaagiza warudi kuuacha uovu. Kama wakisikia na kumtumikia, Watapisha siku zao katika kufanikiwa, Na miaka yao katika furaha. Lakini wasiposikia, wataangamia kwa upanga, Nao watakufa pasipo maarifa. Lakini hao wasiomcha Mungu mioyoni hujiwekea hasira Hawalilii msaada hapo awafungapo. Wao hufa wakingali vijana, Na uhai wao huangamia katikati ya wachafu. Yeye humponya aliyetaabika kwa njia ya taabu yake, Na kuyafunua masikio yao kwa maonevu. Naam, yeye angekuongoza utoke katika msiba Hata mahali penye nafasi, ambapo hapana kizuizi; Na kilichowekwa mezani pako kingejaa mafuta. Lakini umejaa hukumu ya waovu; Hukumu na haki hukushika. Basi ujitunze, isije hasira ikakuvuta hata ukafanya mzaha; Wala usikubali ukuu wa ukombozi ukugeuze. Je! Mali yako itatosha, hata usiwe katika taabu, Au uwezo wote wa nguvu zako? Usiutamani usiku, Wakati watu wakatwapo katika mahali pao. Jitunze, usiutazame uovu; Kwani umeuchagua huo zaidi ya taabu. Tazama, Mungu hutenda makuu kwa uweza wake; Ni nani afundishaye kama yeye? Ni nani aliyemwagiza njia yake? Au ni nani awezaye kusema, Wewe umetenda yasiyo haki? Kumbuka kuitukuza kazi yake, Watu waliyoiimbia. Wanadamu wote wameitazama; Watu huiangalia kwa mbali.
Yobu 36:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena Elihu akaendelea na kusema, Ningojee kidogo nami nitakueleza; Kwa kuwa nikali na maneno kwa ajili ya Mungu. Nitayaleta maarifa yangu kutoka mbali, Nami nitampa haki Muumba wangu. Kwani yakini maneno yangu si ya uongo; Aliyekamilika katika maarifa yu pamoja nawe. Tazama, Mungu ni hodari, wala hamdharau mtu ye yote; Ana uweza katika nguvu za fahamu. Hauhifadhi uhai wa waovu; Lakini huwapa wateswao haki yao. Yeye hawaondolei macho yake wenye haki; Lakini pamoja na wafalme huwaweka Katika viti vya enzi milele, nao hutukuzwa. Nao wakifungwa kwa pingu, Wakitwaliwa kwa kamba za mateso; Ndipo huwaonyesha matendo yao, Na makosa yao, ya kuwa wametenda kwa kujivuna. Yeye huyafunua masikio yao, wasikie maonyo, Na kuwaagiza warudi kuuacha uovu. Kama wakisikia na kumtumikia, Watapisha siku zao katika kufanikiwa, Na miaka yao katika furaha. Lakini wasiposikia, wataangamia kwa upanga, Nao watakufa pasipo maarifa. Lakini hao wasiomcha Mungu mioyoni hujiwekea hasira Hawalilii msaada hapo awafungapo. Wao hufa wakali vijana, Na uhai wao huangamia katikati ya wachafu. Yeye humponya aliyetaabika kwa njia ya taabu yake, Na kuyafunua masikio yao kwa maonevu. Naam, yeye angekuongoza utoke katika msiba Hata mahali penye nafasi, ambapo hapana msonge; Na kilichowekwa mezani pako kingejaa mafuta. Lakini umejaa hukumu ya waovu; Hukumu na haki hukushika. Basi ujitunze, isije hasira ikakuvuta hata ukafanya mzaha; Wala usikubali ukuu wa ukombozi ukugeuze. Je! Mali yako yatatosha, hata usiwe katika taabu, Au uwezo wote wa nguvu zako? Usiutamani usiku, Wakati watu wakatwapo katika mahali pao. Jitunze, usiutazame uovu; Kwani umeuchagua huo zaidi ya taabu. Tazama, Mungu hutenda makuu kwa uweza wake; Ni nani afundishaye kama yeye? Ni nani aliyemwagiza njia yake? Au ni nani awezaye kusema, Wewe umetenda yasiyo haki? Kumbuka kuitukuza kazi yake, Watu waliyoiimbia. Wanadamu wote wameitazama; Watu huiangalia kwa mbali
Yobu 36:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Elihu akaendelea kusema: “Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonesha kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu. Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali, nami nitamhesabia haki Muumba wangu. Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo; mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe. “Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu; ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika kusudi lake. Hawaachi waovu waendelee kuishi, bali huwapa walioteswa haki yao. Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki; huwaketisha penye viti vya utawala pamoja na wafalme, na kuwatukuza milele. Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo, wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso, huwaonesha yale waliyoyatenda, kwamba wametenda dhambi kwa majivuno. Huwafanya wao kusikia maonyo, na huwaagiza kutubu uovu wao. Wakitii na kumtumikia, wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio, na miaka yao katika utoshelevu. Lakini wasiposikiliza, wataangamia kwa upanga, nao watakufa pasipo maarifa. “Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki; hata anapowafunga, hawamwombi msaada. Wanakufa wangali vijana, miongoni mwa mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu. Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao, na kuzungumza nao katika dhiki zao. “Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki, ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi, hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri. Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu; hukumu na haki vimekukamata. Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri; usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa. Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki? Usiutamani usiku uje, ili uwaburute watu mbali na nyumba zao. Jihadhari usigeukie uovu, ambao unaupenda zaidi ya mateso. “Mungu ametukuzwa katika nguvu zake. Ni nani aliye mwalimu kama yeye? Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake, au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’? Kumbuka kuzitukuza kazi zake, ambazo watu wamezisifu katika wimbo. Wanadamu wote wameiona; watu wanaikazia macho kwa mbali.