Yeremia 32:1-25
Yeremia 32:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia, mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Nebukadneza. Wakati huo, majeshi ya mfalme wa Babuloni yalikuwa yakiuzingira mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ukumbi wa walinzi uliokuwa ndani ya ikulu ya mfalme wa Yuda. Maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga Yeremia akisema, “Kwa nini unatabiri na kusema: ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Tazama, mimi nautia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteka. Sedekia, mfalme wa Yuda, hataepa kutiwa mikononi mwa Wakaldayo; hakika atatekwa na mfalme wa Babuloni, ataonana naye uso kwa uso na kuongea naye ana kwa ana. Sedekia atachukuliwa hadi Babuloni, naye atakaa huko mpaka nitakapomchukulia hatua. Hata kama Sedekia atapigana na Wakaldayo, hatashinda.’” Yeremia akasema, Mwenyezi-Mungu alinena nami akasema: “Hanameli, mwana wa baba yako mdogo Shalumu, atakujia na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi, maana wewe ni ndugu yangu kabisa, na unayo haki ya kulikomboa.’” Kisha binamu yangu Hanameli alinijia katika ukumbi wa walinzi kama alivyonifahamisha Mwenyezi-Mungu, akaniambia, “Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini maana wewe una haki ya kulikomboa. Linunue kwa faida yako.” Ndipo nilipotambua kwamba lilikuwa kweli neno la Mwenyezi-Mungu. Basi, nililinunua shamba hilo lililoko Anathothi, kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nikamlipa bei yake shekeli kumi na saba za fedha. Nikaitia sahihi hati ya kumiliki, nikaipiga mhuri, nikawaita mashahidi na kuipima ile fedha katika mizani. Kisha, nilichukua ile hati ya kumiliki niliyoipiga mhuri, ambayo ilikuwa na masharti na kanuni, pamoja na nakala nyingine iliyokuwa wazi. Nilimpa hiyo hati ya ununuzi Baruku mwana wa Neria mwana wa Maaseya, mbele ya binamu yangu Hanameli na mashahidi waliokuwa wametia sahihi hati ya ununuzi, na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ukumbi wa walinzi. Mbele ya watu wote hao, nilimpa Baruku maagizo yafuatayo: Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Chukua hati hizi zote mbili, hati hii ya kumiliki shamba iliyotiwa sahihi, na hii nyingine iliyo wazi, uziweke katika chungu ili zipate kuhifadhiwa kwa muda mrefu.” Maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nyumba na mashamba, pamoja na mashamba ya mizabibu katika nchi hii yatanunuliwa tena.” Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria, hati ya kumiliki shamba nilimwomba Mwenyezi-Mungu nikisema: Ee Mwenyezi-Mungu, ni wewe ambaye kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu, umeziumba mbingu na dunia; hakuna kisichowezekana kwako. Wewe unaonesha fadhili zako kwa maelfu ya watu; lakini pia unawaadhibu watu kwa sababu ya dhambi za wazee wao. Wewe ni Mungu mkuu, mwenye nguvu, Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lako. Wewe unapanga kwa hekima na unafanya maajabu; njia za watu wote ziko wazi mbele yako, unamlipa kila mmoja kadiri ya njia zake na matendo yake. Katika nchi ya Misri ulifanya maajabu, ukatenda miujiza, na unaendelea kufanya hivyo mpaka leo miongoni mwa Waisraeli na katika mataifa mengine pia, jambo ambalo limekufanya ujulikane kila mahali. Kwa maajabu na miujiza uliyowatisha nayo Wamisri, uliwatoa watu wako Misri kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu. Uliwapa nchi hii ambayo uliahidi kuwapa wazee wao, nchi inayotiririka maziwa na asali. Nao walifika, wakaitwa na kuimiliki. Lakini wao hawakukusikiliza, wala hawakufuata sheria zako. Hawakutenda mambo uliyoamuru. Ndiyo maana utawafanya wapatwe na balaa hii. Tazama, Wakaldayo wamechimba mahandaki kuuzunguka mji; wameuzingira ili wapate kuuteka; wanaushambulia. Vita, njaa na maradhi vitaufanya mji utekwe na watu hao. Kweli mambo uliyotabiri yametokea. Unaona mwenyewe. Lakini, ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe uliyeniambia: “Nunua shamba kwa fedha na kuweka mashahidi,” ingawa mji wenyewe umetekwa na Wakaldayo.
Yeremia 32:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, katika mwaka wa kumi wa Sedekia, mfalme wa Yuda, nao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa Nebukadneza. Basi, wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli liliuzunguka Yerusalemu; na Yeremia, nabii, alikuwa amefungwa ndani ya uwanja wa walinzi, uliokuwa katika nyumba ya mfalme wa Yuda. Kwa maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga, akisema, Kwa nini unatabiri, na kusema, BWANA asema hivi, Angalia, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atautwaa; tena, Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona kutoka katika mikono ya Wakaldayo, lakini hakika yake atatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, atanena naye ana kwa ana, na watatazamana macho kwa macho; naye atamchukua Sedekia mpaka Babeli, naye atakuwako huko hadi nitakapomjia, asema BWANA; mjapopigana na Wakaldayo hamtafanikiwa. Yeremia akasema, Neno la BWANA limenijia, kusema, Tazama, Hanameli, mwana wa Shalumu, mjomba wako, atakujia, akisema, Jinunulie shamba langu lililoko Anathothi; maana haki ya ukombozi ni yako, ulinunue. Basi Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akanijia ndani ya ukumbi wa walinzi, sawasawa na lile neno la BWANA, akaniambia, Tafadhali, ulinunue shamba langu lililoko Anathothi, katika nchi ya Benyamini; maana haki ya urithi ni yako, na haki ya ukombozi ni yako; ujinunulie. Ndipo nikajua kama neno hili ni neno la BWANA. Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha. Nami nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga mhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani. Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa mhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi; na ile hati ya kununua nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mbele ya uso wa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, na mbele ya mashahidi wale walioitia sahihi hati ya kununua, mbele ya Wayahudi wote walioketi katika ukumbi wa walinzi. Nami nikamwagiza Baruku mbele yao, nikisema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Twaa hati hizi, hati hii ya kununua, hati hii iliyopigwa mhuri, na hii iliyo wazi pia, ukazitie katika chombo cha udongo, zipate kukaa siku nyingi. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyumba na mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii. Hata nikiisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, hati ile ya kununua, nilimwomba BWANA, nikisema, Aa! Bwana MUNGU, tazama, wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza; wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, BWANA wa majeshi ndilo jina lake; mkuu wa mashauri, muweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake, wewe uliyeweka ishara na ajabu katika nchi ya Misri hata siku hii ya leo, katika Israeli na kati ya watu wengine; na kujifanyia jina kama ilivyo leo; ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mkuu; ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi itiririkayo maziwa na asali; nao wakaingia, wakaimiliki; lakini hawakuitii sauti yako, wala hawakuenda katika sheria yako; hawakutenda neno lolote katika haya uliyowaagiza wayatende; basi, kwa sababu hii umeleta juu yao mabaya haya yote; angalia maboma haya; wameujia mji huu ili kuutwaa; na mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo wanaopigana nao, kwa sababu ya upanga, na njaa, na tauni; na hayo uliyosema yamekuwa; na, tazama, wewe unayaona. Nawe, Ee Bwana MUNGU, umeniambia, Jinunulie shamba lile kwa fedha, ukawaite mashahidi; iwapo mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo; je! Itakuwaje?
Yeremia 32:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, katika mwaka wa kumi wa Sedekia, mfalme wa Yuda, nao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza. Basi, wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli liliuzunguka Yerusalemu; na Yeremia, nabii, alikuwa amefungwa ndani ya uwanda wa walinzi, uliokuwa katika nyumba ya mfalme wa Yuda. Kwa maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga, akisema, Kwa nini unatabiri, na kusema, BWANA asema hivi, Angalia, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atautwaa; tena, Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona kutoka katika mikono ya Wakaldayo, lakini hakika yake atatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, atanena naye mdomo kwa mdomo, na macho yake yatatazama macho yake; naye atamchukua Sedekia mpaka Babeli, naye atakuwako huko hata nitakapomjilia, asema BWANA; mjapopigana na Wakaldayo hamtafanikiwa. Yeremia akasema, Neno la BWANA limenijia, kusema, Tazama, Hanameli, mwana wa Shalumu, mjomba wako, atakujia, akisema, Jinunulie shamba langu lililoko Anathothi; maana haki ya ukombozi ni yako, ulinunue. Basi Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akanijia ndani ya uwanda wa walinzi, sawasawa na lile neno la BWANA, akaniambia, Tafadhali, ulinunue shamba langu lililoko Anathothi, katika nchi ya Benyamini; maana haki ya urithi ni yako, na haki ya ukombozi ni yako; ujinunulie. Ndipo nikajua kama neno hili ni neno la BWANA. Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha. Nami nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga muhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani. Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa muhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi; na ile hati ya kununua nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mbele ya uso wa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, na mbele ya mashahidi wale walioitia sahihi hati ya kununua, mbele ya Wayahudi wote walioketi katika uwanda wa walinzi. Nami nikamwagiza Baruku mbele yao, nikisema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Twaa hati hizi, hati hii ya kununua, hati hii iliyopigwa muhuri, na hii iliyo wazi pia, ukazitie katika chombo cha udongo, zipate kukaa siku nyingi. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyumba na mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii. Hata nikiisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, hati ile ya kununua, nalimwomba BWANA, nikisema, Aa! Bwana MUNGU, tazama, wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza; wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, BWANA wa majeshi ndilo jina lake; mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake, wewe uliyeweka ishara na ajabu katika nchi ya Misri hata siku hii ya leo, katika Israeli na kati ya watu wengine; na kujifanyia jina kama ilivyo leo; ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mkuu; ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi iliyojaa maziwa na asali; nao wakaingia, wakaimiliki; lakini hawakuitii sauti yako, wala hawakuenda katika sheria yako; hawakutenda neno lo lote katika haya uliyowaagiza wayatende; basi, kwa sababu hii umeleta juu yao mabaya haya yote; angalia maboma haya; wameujia mji huu ili kuutwaa; na mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo wanaopigana nao, kwa sababu ya upanga, na njaa, na tauni; na hayo uliyosema yamekuwa; na, tazama, wewe unayaona. Nawe, Ee Bwana MUNGU, umeniambia, Jinunulie shamba lile kwa fedha, ukawaite mashahidi; iwapo mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo; je! Itakuwaje?
Yeremia 32:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa BWANA, katika mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Nebukadneza. Wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli lilikuwa limeuzingira mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi katika jumba la kifalme la Yuda. Basi Sedekia mfalme wa Yuda alikuwa amemfunga huko akisema, “Kwa nini unatabiri hivyo? Wewe unasema, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Ninakaribia kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteka. Sedekia mfalme wa Yuda hataweza kuponyoka mikononi mwa Wakaldayo, lakini kwa hakika atatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atazungumza naye ana kwa ana na kumwona kwa macho yake mwenyewe. Atamchukua Sedekia hadi Babeli, mahali atakapoishi hadi nitakapomshughulikia, asema BWANA. Kama utapigana dhidi ya Wakaldayo, hutashinda.’ ” Yeremia akasema, “Neno la BWANA lilinijia kusema: Hanameli mwana wa Shalumu mjomba wako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulikomboa.’ “Kisha, kama BWANA alivyosema, binamu yangu Hanameli alinijia katika ua wa walinzi na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini. Kwa kuwa ni haki yako kulikomboa na kulimiliki, jinunulie.’ “Nilijua kwamba hili lilikuwa neno la BWANA. Hivyo nikalinunua shamba hilo lililoko Anathothi kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nami nikampimia shekeli kumi na saba za fedha. Nikatia sahihi na kuweka muhuri hati ya kumiliki, nikaweka mashahidi, na kupima ile fedha kwenye mizani. Nikachukua ile hati ya kununulia, nakala iliyotiwa muhuri yenye makubaliano na masharti, pia pamoja na ile nakala isiyo na muhuri, nami nikampa Baruku mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, hati hii mbele ya binamu yangu Hanameli, na mbele ya mashahidi waliokuwa wameweka sahihi kwenye hati hii na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ua wa walinzi. “Nilimpa Baruku maelezo haya mbele yao: ‘Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli: Chukua hati hizi, yaani nakala zote zenye muhuri na zisizo na muhuri za hati ya kununulia, na uziweke kwenye gudulia la udongo wa mfinyanzi ili zidumu kwa muda mrefu. Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli: Nyumba, mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.’ “Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria hii hati ya kununulia, nilimwomba BWANA: “Ee BWANA Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza. Wewe huonesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako ni BWANA wa majeshi, mashauri yako ni makuu, na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake, na kwa kadri ya matendo yake. Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri, na unafanya hivyo hadi leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo hadi leo. Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa utisho mkuu. Uliwapa nchi hii uliyokuwa umeapa kuwapa baba zao, nchi inayotiririka maziwa na asali. Waliingia na kuimiliki, lakini hawakukutii wala kuifuata sheria yako. Hawakufanya kile ulichowaamuru kufanya. Hivyo ukaleta maafa haya yote juu yao. “Tazama jinsi jeshi lilivyouzingira mji huu ili kuuteka. Kwa sababu ya upanga, njaa, na tauni, mji utatiwa mkononi mwa Wakaldayo wanaoushambulia. Ulilolisema limetokea kama unavyoona. Ingawa mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo, wewe, Ee BWANA Mwenyezi, uliniambia, ‘Nunua shamba kwa fedha mbele ya mashahidi.’ ”