Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 32:1-25

Yeremia 32:1-25 BHN

Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia, mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Nebukadneza. Wakati huo, majeshi ya mfalme wa Babuloni yalikuwa yakiuzingira mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ukumbi wa walinzi uliokuwa ndani ya ikulu ya mfalme wa Yuda. Maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga Yeremia akisema, “Kwa nini unatabiri na kusema: ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Tazama, mimi nautia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteka. Sedekia, mfalme wa Yuda, hataepa kutiwa mikononi mwa Wakaldayo; hakika atatekwa na mfalme wa Babuloni, ataonana naye uso kwa uso na kuongea naye ana kwa ana. Sedekia atachukuliwa hadi Babuloni, naye atakaa huko mpaka nitakapomchukulia hatua. Hata kama Sedekia atapigana na Wakaldayo, hatashinda.’” Yeremia akasema, Mwenyezi-Mungu alinena nami akasema: “Hanameli, mwana wa baba yako mdogo Shalumu, atakujia na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi, maana wewe ni ndugu yangu kabisa, na unayo haki ya kulikomboa.’” Kisha binamu yangu Hanameli alinijia katika ukumbi wa walinzi kama alivyonifahamisha Mwenyezi-Mungu, akaniambia, “Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini maana wewe una haki ya kulikomboa. Linunue kwa faida yako.” Ndipo nilipotambua kwamba lilikuwa kweli neno la Mwenyezi-Mungu. Basi, nililinunua shamba hilo lililoko Anathothi, kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nikamlipa bei yake shekeli kumi na saba za fedha. Nikaitia sahihi hati ya kumiliki, nikaipiga mhuri, nikawaita mashahidi na kuipima ile fedha katika mizani. Kisha, nilichukua ile hati ya kumiliki niliyoipiga mhuri, ambayo ilikuwa na masharti na kanuni, pamoja na nakala nyingine iliyokuwa wazi. Nilimpa hiyo hati ya ununuzi Baruku mwana wa Neria mwana wa Maaseya, mbele ya binamu yangu Hanameli na mashahidi waliokuwa wametia sahihi hati ya ununuzi, na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ukumbi wa walinzi. Mbele ya watu wote hao, nilimpa Baruku maagizo yafuatayo: Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Chukua hati hizi zote mbili, hati hii ya kumiliki shamba iliyotiwa sahihi, na hii nyingine iliyo wazi, uziweke katika chungu ili zipate kuhifadhiwa kwa muda mrefu.” Maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nyumba na mashamba, pamoja na mashamba ya mizabibu katika nchi hii yatanunuliwa tena.” Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria, hati ya kumiliki shamba nilimwomba Mwenyezi-Mungu nikisema: Ee Mwenyezi-Mungu, ni wewe ambaye kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu, umeziumba mbingu na dunia; hakuna kisichowezekana kwako. Wewe unaonesha fadhili zako kwa maelfu ya watu; lakini pia unawaadhibu watu kwa sababu ya dhambi za wazee wao. Wewe ni Mungu mkuu, mwenye nguvu, Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lako. Wewe unapanga kwa hekima na unafanya maajabu; njia za watu wote ziko wazi mbele yako, unamlipa kila mmoja kadiri ya njia zake na matendo yake. Katika nchi ya Misri ulifanya maajabu, ukatenda miujiza, na unaendelea kufanya hivyo mpaka leo miongoni mwa Waisraeli na katika mataifa mengine pia, jambo ambalo limekufanya ujulikane kila mahali. Kwa maajabu na miujiza uliyowatisha nayo Wamisri, uliwatoa watu wako Misri kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu. Uliwapa nchi hii ambayo uliahidi kuwapa wazee wao, nchi inayotiririka maziwa na asali. Nao walifika, wakaitwa na kuimiliki. Lakini wao hawakukusikiliza, wala hawakufuata sheria zako. Hawakutenda mambo uliyoamuru. Ndiyo maana utawafanya wapatwe na balaa hii. Tazama, Wakaldayo wamechimba mahandaki kuuzunguka mji; wameuzingira ili wapate kuuteka; wanaushambulia. Vita, njaa na maradhi vitaufanya mji utekwe na watu hao. Kweli mambo uliyotabiri yametokea. Unaona mwenyewe. Lakini, ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe uliyeniambia: “Nunua shamba kwa fedha na kuweka mashahidi,” ingawa mji wenyewe umetekwa na Wakaldayo.

Soma Yeremia 32