Yeremia 32:1-25
Yeremia 32:1-25 NENO
Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa BWANA, katika mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Nebukadneza. Wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli lilikuwa limeuzingira mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi katika jumba la kifalme la Yuda. Basi Sedekia mfalme wa Yuda alikuwa amemfunga huko akisema, “Kwa nini unatabiri hivyo? Wewe unasema, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Ninakaribia kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteka. Sedekia mfalme wa Yuda hataweza kuponyoka mikononi mwa Wakaldayo, lakini kwa hakika atatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atazungumza naye ana kwa ana na kumwona kwa macho yake mwenyewe. Atamchukua Sedekia hadi Babeli, mahali atakapoishi hadi nitakapomshughulikia, asema BWANA. Kama utapigana dhidi ya Wakaldayo, hutashinda.’ ” Yeremia akasema, “Neno la BWANA lilinijia kusema: Hanameli mwana wa Shalumu mjomba wako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulikomboa.’ “Kisha, kama BWANA alivyosema, binamu yangu Hanameli alinijia katika ua wa walinzi na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini. Kwa kuwa ni haki yako kulikomboa na kulimiliki, jinunulie.’ “Nilijua kwamba hili lilikuwa neno la BWANA. Hivyo nikalinunua shamba hilo lililoko Anathothi kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nami nikampimia shekeli kumi na saba za fedha. Nikatia sahihi na kuweka muhuri hati ya kumiliki, nikaweka mashahidi, na kupima ile fedha kwenye mizani. Nikachukua ile hati ya kununulia, nakala iliyotiwa muhuri yenye makubaliano na masharti, pia pamoja na ile nakala isiyo na muhuri, nami nikampa Baruku mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, hati hii mbele ya binamu yangu Hanameli, na mbele ya mashahidi waliokuwa wameweka sahihi kwenye hati hii na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ua wa walinzi. “Nilimpa Baruku maelezo haya mbele yao: ‘Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli: Chukua hati hizi, yaani nakala zote zenye muhuri na zisizo na muhuri za hati ya kununulia, na uziweke kwenye gudulia la udongo wa mfinyanzi ili zidumu kwa muda mrefu. Kwa kuwa hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli: Nyumba, mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.’ “Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria hii hati ya kununulia, nilimwomba BWANA: “Ee BWANA Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza. Wewe huonesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako ni BWANA wa majeshi, mashauri yako ni makuu, na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake, na kwa kadri ya matendo yake. Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri, na unafanya hivyo hadi leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo hadi leo. Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa utisho mkuu. Uliwapa nchi hii uliyokuwa umeapa kuwapa baba zao, nchi inayotiririka maziwa na asali. Waliingia na kuimiliki, lakini hawakukutii wala kuifuata sheria yako. Hawakufanya kile ulichowaamuru kufanya. Hivyo ukaleta maafa haya yote juu yao. “Tazama jinsi jeshi lilivyouzingira mji huu ili kuuteka. Kwa sababu ya upanga, njaa, na tauni, mji utatiwa mkononi mwa Wakaldayo wanaoushambulia. Ulilolisema limetokea kama unavyoona. Ingawa mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo, wewe, Ee BWANA Mwenyezi, uliniambia, ‘Nunua shamba kwa fedha mbele ya mashahidi.’ ”