Isaya 41:1-29
Isaya 41:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu asema hivi: “Enyi wakazi wa mbali nyamazeni mnisikilize! Enyi mataifa jipeni nguvu; jitokezeni mkatoe hoja zenu, na tuje pamoja kwa hukumu. “Nani, ila mimi, aliyemwita shujaa toka mashariki, mtu ambaye hupata ushindi popote aendako? Mimi huyatia mataifa makuchani mwake, naye huwaponda wafalme chini ya miguu yake! Upanga wake huwafanya kuwa kama vumbi, kwa upinde wake huwapeperusha kama makapi. Yeye huwafuatia na kupita salama; huenda kasi kana kwamba hagusi chini. Nani aliyefanya yote haya yatendeke? Ni nani aliyepanga wakati wa kila tukio? Mimi Mwenyezi-Mungu nipo tangu mwanzo, mimi nitakuwapo hata milele. “Wakazi wa mbali wameona niliyotenda, wakaogopa; dunia yote inatetemeka kwa hofu. Watu wote wamekusanyika, wakaja. Kila mmoja anamhimiza mwenzake akisema, ‘Haya! Jipe moyo!’ Fundi anamhimiza mfua dhahabu, naye alainishaye sanamu kwa nyundo, anamhimiza anayeiunga kwa misumari. Wote wanasema, ‘Imeungika vizuri sana!’ Kisha wanaifunga kwa misumari isitikisike. “Sikiliza ewe Israeli, mtumishi wangu, wewe, Yakobo ambaye nimekuchagua, wewe mzawa wa Abrahamu, rafiki yangu; wewe niliyekuleta toka miisho ya dunia, wewe niliyekuambia: ‘Wewe u mtumishi wangu; mimi sikukutupa, bali nilikuchagua.’ Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi. “Naam! Wote waliokuwakia hasira, wataaibishwa na kupata fedheha. Wote wanaopingana nawe, watakuwa si kitu na kuangamia. Utawatafuta hao wanaopingana nawe, lakini watakuwa wameangamia. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ndimi ninayetegemeza mkono wako. Mimi ndimi ninayekuambia: ‘Usiogope, nitakusaidia.’” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wa Yakobo dhaifu kama mdudu, enyi Waisraeli, msiogope! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema nitawasaidia. Mimi ni Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli. Nitawafanya muwe kama chombo cha kupuria, chenye meno mapya na makali. Mtaipura milima na kuipondaponda; vilima mtavisagasaga kama makapi. Mtaipepeta milima hiyo, nao upepo utaipeperushia mbali, naam, dhoruba itaitawanya huko na huko. Nanyi mtafurahi kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu; mtaona fahari kwa sababu yangu Mungu Mtakatifu wa Israeli. “Maskini na fukara wakitafuta maji wasipate, wakiwa wamekauka koo kwa kiu, mimi Mwenyezi-Mungu nitawajibu; mimi Mungu wa Israeli, sitawaacha. Nitabubujisha mito kwenye milima mikavu, na chemchemi katika mabonde. Nitaigeuza nyika kuwa bwawa la maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Nitapanda miti huko nyikani: Mierezi, mikakaya, mijohoro, na mizeituni; nitaweka huko jangwani: Miberoshi, mivinje na misonobari. Watu wataona jambo hilo, nao watatambua na kuelewa kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nimetenda hayo, mimi Mtakatifu wa Israeli nimefanya jambo hilo.” Mwenyezi-Mungu, Mfalme wa Yakobo, asema: “Enyi miungu ya mataifa, njoni mtoe hoja zenu! Leteni hoja zenu, mtuambie yatakayotukia. Tuambieni matukio ya kwanza yalikuwa yapi nasi tutayatafakari moyoni. Au tutangazieni yajayo, tujue yatakayokuja. Tuambieni yatakayotokea baadaye, nasi tujue basi kama nyinyi ni miungu. Fanyeni kitu chochote, chema au kibaya, ili tutishike na kuogopa. Hakika, nyinyi si kitu kabisa. hamwezi kufanya chochote kile. Anayechagua kuwaabudu nyinyi ni chukizo. “Nimechochea mtu toka kaskazini, naye amekuja; naam, nimemchagua mtu toka mashariki, naye atalitamka jina langu. Yeye atawakanyaga wafalme kama tope, kama vile mfinyanzi apondavyo udongo wake. Nani aliyebashiri haya tangu mwanzo, hata sisi tupate kuyatambua? Nani aliyetangulia kuyatangaza, ili sasa tuseme, alisema ukweli? Hakuna hata mmoja wenu aliyeyataja, wala hakuna aliyesikia maneno yenu. Mimi ni yule wa kwanza, niliyetangaza kwa Siyoni, nikapeleka Yerusalemu mjumbe wa habari njema. Nimeangalia kwa makini sana, lakini simwoni yeyote yule; hamna yeyote kati ya hao miungu awezaye kushauri; nikiuliza hakuna awezaye kunijibu. La! Miungu hiyo yote ni udanganyifu, haiwezi kufanya chochote; sanamu zao za kusubu ni upuuzi.
Isaya 41:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu. Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake. Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake. Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye. Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja. Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Jipe moyo. Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike. Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Abrahamu, rafiki yangu; wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kulia wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kulia, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema BWANA, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli. Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, BWANA, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji. Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja; ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa BWANA ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba. Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo. Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; watuoneshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye. Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu; naam, tendeni mema au tendeni mabaya, ili tujipime, tukaone pamoja. Tazameni, ninyi si kitu, tena kazi yenu si kitu; awachaguaye ninyi ni chukizo. Nimemwinua mtu toka kaskazini, naye amekuja; toka maawio ya jua amekuja anitajaye jina langu; naye atawakanyaga watawala kama akanyagaye matope, na kama mfinyanzi apondaye udongo. Ni nani aliyeihubiri habari tokea mwanzo, tupate kuijua? Na tokea zamani, tupate kusema, Yeye ni mwenye haki? Naam, hapana hata mmoja aliyetujulisha; naam, hapana hata mmoja aliyetuonesha; naam, hapana hata mmoja aliyesikia maneno yenu. Mimi kwanza nitauambia Sayuni, Tazama; hawa ndio; nami nitampa Yerusalemu mletaji wa habari njema. Na nitazamapo, hapana mtu, hata katika watu hao hapana mshauri mmoja, ambaye, nikimwuliza, aweza kunijibu neno. Tazama, hao wote ni ubatili; kazi zao si kitu; sanamu zao ni upepo mtupu.
Isaya 41:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu. Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake. Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake. Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye. Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja. Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Uwe na moyo mkuu. Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike. Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu; wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema BWANA, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli. Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, BWANA, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji. Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja; ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa BWANA ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba. Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo. Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; watuonyeshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye. Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu; naam, tendeni mema au tendeni mabaya, ili tujipime, tukaone pamoja. Tazameni, ninyi si kitu, tena kazi yenu si kitu; awachaguaye ninyi ni chukizo. Nimemwinua mtu toka kaskazini, naye amekuja; toka maawio ya jua amekuja anitajaye jina langu; naye atawajilia maliwali kama akanyagaye matope, na kama mfinyanzi afinyangaye udongo. Ni nani aliyeihubiri habari tokea mwanzo, tupate kuijua? Na tokea zamani, tupate kusema, Yeye ni mwenye haki? Naam, hapana hata mmoja aliyetujulisha; naam, hapana hata mmoja aliyetuonyesha; naam, hapana hata mmoja aliyesikia maneno yenu. Mimi kwanza nitauambia Sayuni, Tazama; hawa ndio; nami nitampa Yerusalemu mletaji wa habari njema. Na nitazamapo, hapana mtu, hata katika watu hao hapana mshauri mmoja, ambaye, nikimwuliza, aweza kunijibu neno. Tazama, hao wote ni ubatili; kazi zao si kitu; sanamu zao ni upepo na fujo.
Isaya 41:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Nyamazeni kimya mbele zangu, enyi visiwa! Mataifa na wafanye upya nguvu zao! Wao na wajitokeze, kisha waseme, tukutane pamoja mahali pa hukumu. “Ni nani aliyemchochea mmoja kutoka mashariki, akimwita katika haki kwa utumishi wake? Huyatia mataifa mkononi mwake, na kuwatiisha wafalme mbele zake. Huwafanya kuwa mavumbi kwa upanga wake, huwafanya makapi yapeperushwayo na upepo kwa upinde wake. Huwafuatia na kuendelea salama, katika njia ambayo miguu yake haijawahi kupita. Ni nani aliyefanya jambo hili na kulitimiliza, akiita vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, ni wa kwanza, nami nitakuwa pamoja na wa mwisho: Mimi ndiye.” Visiwa vimeliona na kuogopa, miisho ya dunia inatetemeka. Wanakaribia na kuja mbele, kila mmoja humsaidia mwingine na kusema kwa ndugu yake, “Uwe hodari!” Fundi humtia moyo sonara, yeye alainishaye kwa nyundo humhimiza yeye agongeaye kwenye fuawe. Humwambia yeye aunganishaye, “Ni kazi njema.” Naye huikaza sanamu kwa misumari ili isitikisike. “Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu, Yakobo, niliyemchagua, ninyi wazao wa Abrahamu rafiki yangu, nilikuchukua toka miisho ya dunia, nilikuita kutoka pembe zake za mbali. Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’; nimekuchagua, wala sikukukataa. Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu na kukusaidia; nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu. “Wote walioona hasira dhidi yako hakika wataaibika na kutahayarika, wale wakupingao watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia. Ingawa utawatafuta adui zako, hutawaona. Wale wanaopigana vita dhidi yako watakuwa kama vile si kitu kabisa. Kwa maana Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, nikushikaye mkono wako wa kuume na kukuambia, Usiwe na hofu, nitakusaidia. Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu, ee Israeli uliye mdogo, kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema BWANA, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. “Tazama, nitakufanya chombo cha kupuria, kipya na chenye makali, chenye meno mengi. Utaipura milima na kuiponda na kuvifanya vilima kuwa kama makapi. Utaipepeta, nao upepo utaichukua, dhoruba itaipeperushia mbali. Bali wewe utajifurahisha katika BWANA na katika utukufu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. “Maskini na wahitaji wanatafuta maji, lakini hayapo, ndimi zao zimekauka kwa kiu. Lakini Mimi BWANA nitawajibu, Mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. Nitaifanya mito itiririke juu ya vilima vilivyo kame, nazo chemchemi ndani ya mabonde. Nitaligeuza jangwa liwe mabwawa ya maji, nayo ardhi iliyokauka kuwa chemchemi za maji. Katika jangwa nitaotesha mwerezi, mshita, mhadasi na mzeituni. Nitaweka misunobari, mivinje na misanduku pamoja huko nyikani, ili watu wapate kuona na kujua, wapate kufikiri na kuelewa, kwamba mkono wa BWANA umetenda hili, kwamba yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ndiye alilifanya.” BWANA asema, “Leta shauri lako. Toa hoja yako,” asema Mfalme wa Yakobo. “Leteni sanamu zenu zituambie ni nini kitakachotokea. Tuambieni mambo ya zamani yalikuwa nini, ili tupate kuyatafakari na kujua matokeo yake ya mwisho. Au tutangazieni mambo yatakayokuja, tuambieni ni nini kitakachotokea baadaye, ili tupate kujua kuwa ninyi ni miungu. Fanyeni jambo lolote zuri au baya, ili tupate kutishika na kujazwa na hofu. Lakini ninyi ni zaidi ya bure kabisa, na kazi zenu hazifai kitu kabisa; yeye awachaguaye ni chukizo sana. “Nimemchochea mtu mmoja kutoka kaskazini, naye yuaja, mmoja toka mawio ya jua aliitaye Jina langu. Huwakanyaga watawala kana kwamba ni matope, kama mfinyanzi akanyagavyo udongo wa kufinyangia. Ni nani aliyenena hili tokea mwanzoni, ili tupate kujua, au kabla, ili tuweze kusema, ‘Alikuwa mwenye haki’? Hakuna aliyenena hili, hakuna aliyetangulia kusema hili, hakuna yeyote aliyesikia maneno kutoka kwenu. Nilikuwa wa kwanza kumwambia Sayuni, ‘Tazama, wako hapa!’ Nilimpa Yerusalemu mjumbe wa habari njema. Ninatazama, lakini hakuna yeyote: hakuna yeyote miongoni mwao awezaye kutoa shauri, hakuna yeyote wa kutoa jibu wakati ninapowauliza. Tazama, wote ni ubatili! Matendo yao ni bure; vinyago vyao ni upepo mtupu na machafuko.