Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 41

41
Mungu anaahidi kuisaidia Israeli
1Mungu asema hivi:
“Enyi wakazi wa mbali nyamazeni mnisikilize!
Enyi mataifa jipeni nguvu;
jitokezeni mkatoe hoja zenu,
na tuje pamoja kwa hukumu.
2“Nani, ila mimi, aliyemwita shujaa toka mashariki,
mtu ambaye hupata ushindi popote aendako?
Mimi huyatia mataifa makuchani mwake,
naye huwaponda wafalme chini ya miguu yake!
Upanga wake huwafanya kuwa kama vumbi,
kwa upinde wake huwapeperusha kama makapi.
3Yeye huwafuatia na kupita salama;
huenda kasi kana kwamba hagusi chini.
4Nani aliyefanya yote haya yatendeke?
Ni nani aliyepanga wakati wa kila tukio?
Mimi Mwenyezi-Mungu nipo tangu mwanzo,
mimi nitakuwapo hata milele.
5“Wakazi wa mbali wameona niliyotenda, wakaogopa;
dunia yote inatetemeka kwa hofu.
Watu wote wamekusanyika, wakaja.
6Kila mmoja anamhimiza mwenzake akisema,
‘Haya! Jipe moyo!’
7Fundi anamhimiza mfua dhahabu,
naye alainishaye sanamu kwa nyundo,
anamhimiza anayeiunga kwa misumari.
Wote wanasema, ‘Imeungika vizuri sana!’
Kisha wanaifunga kwa misumari isitikisike.
8 #41:8 Taz Kumb 20:7; Yak 2:23 “Sikiliza ewe Israeli, mtumishi wangu,
wewe, Yakobo ambaye nimekuchagua,
wewe mzawa wa Abrahamu, rafiki yangu;
9wewe niliyekuleta toka miisho ya dunia,
wewe niliyekuambia: ‘Wewe u mtumishi wangu;
mimi sikukutupa, bali nilikuchagua.’
10Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe.
Usifadhaike, mimi ni Mungu wako.
Nitakuimarisha na kukusaidia;
nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.
11“Naam! Wote waliokuwakia hasira,
wataaibishwa na kupata fedheha.
Wote wanaopingana nawe,
watakuwa si kitu na kuangamia.
12Utawatafuta hao wanaopingana nawe,
lakini watakuwa wameangamia.
13Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
ndimi ninayetegemeza mkono wako.
Mimi ndimi ninayekuambia:
‘Usiogope, nitakusaidia.’”
14Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Enyi watu wa Yakobo dhaifu kama mdudu,
enyi Waisraeli, msiogope!
Mimi Mwenyezi-Mungu nasema nitawasaidia.
Mimi ni Mkombozi wenu,
Mtakatifu wa Israeli.
15Nitawafanya muwe kama chombo cha kupuria,
chenye meno mapya na makali.
Mtaipura milima na kuipondaponda;
vilima mtavisagasaga kama makapi.
16Mtaipepeta milima hiyo,
nao upepo utaipeperushia mbali,
naam, dhoruba itaitawanya huko na huko.
Nanyi mtafurahi kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu;
mtaona fahari kwa sababu yangu
Mungu Mtakatifu wa Israeli.
17“Maskini na fukara wakitafuta maji wasipate,
wakiwa wamekauka koo kwa kiu,
mimi Mwenyezi-Mungu nitawajibu;
mimi Mungu wa Israeli, sitawaacha.
18Nitabubujisha mito kwenye milima mikavu,
na chemchemi katika mabonde.
Nitaigeuza nyika kuwa bwawa la maji,
na nchi kame kuwa chemchemi za maji.
19Nitapanda miti huko nyikani:
Mierezi, mikakaya, mijohoro, na mizeituni;
nitaweka huko jangwani:
Miberoshi, mivinje na misonobari.
20Watu wataona jambo hilo,
nao watatambua na kuelewa kwamba
mimi Mwenyezi-Mungu nimetenda hayo,
mimi Mtakatifu wa Israeli nimefanya jambo hilo.”
Mwenyezi-Mungu aipuuza miungu ya uongo
21Mwenyezi-Mungu, Mfalme wa Yakobo, asema:
“Enyi miungu ya mataifa,
njoni mtoe hoja zenu!
22Leteni hoja zenu, mtuambie yatakayotukia.
Tuambieni matukio ya kwanza yalikuwa yapi
nasi tutayatafakari moyoni.
Au tutangazieni yajayo,
tujue yatakayokuja.
23Tuambieni yatakayotokea baadaye,
nasi tujue basi kama nyinyi ni miungu.
Fanyeni kitu chochote, chema au kibaya,
ili tutishike na kuogopa.
24Hakika, nyinyi si kitu kabisa.
hamwezi kufanya chochote kile.
Anayechagua kuwaabudu nyinyi ni chukizo.
25“Nimechochea mtu toka kaskazini,
naye amekuja;
naam, nimemchagua mtu toka mashariki,
naye atalitamka jina langu.
Yeye atawakanyaga wafalme kama tope,
kama vile mfinyanzi apondavyo udongo wake.
26Nani aliyebashiri haya tangu mwanzo,
hata sisi tupate kuyatambua?
Nani aliyetangulia kuyatangaza,
ili sasa tuseme, alisema ukweli?
Hakuna hata mmoja wenu aliyeyataja,
wala hakuna aliyesikia maneno yenu.
27Mimi ni yule wa kwanza, niliyetangaza kwa Siyoni,
nikapeleka Yerusalemu mjumbe wa habari njema.
28Nimeangalia kwa makini sana,
lakini simwoni yeyote yule;
hamna yeyote kati ya hao miungu awezaye kushauri;
nikiuliza hakuna awezaye kunijibu.
29La! Miungu hiyo yote ni udanganyifu,
haiwezi kufanya chochote;
sanamu zao za kusubu ni upuuzi.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 41: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha