Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 41

41
Israeli kuhakikishiwa msaada wa Mungu
1Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu. 2#Isa 46:11; 45:1 Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake. 3Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake. 4#Isa 44:7; 43:10; 48:12; Mdo 15:18; Ufu 1:11,17 Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, BWANA, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye. 5Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja. 6Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Jipe moyo. 7Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike.
8 # Mwa 18:19; Neh 9:7; 2 Nya 20:7; Yak 2:23 Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Abrahamu, rafiki yangu; 9wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; 10#Kum 31:6; Rum 8:31 usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kulia wa haki yangu. 11#Kut 23:22; Zek 12:3 Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. 12Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. 13Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kulia, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. 14#Ayu 19:25 Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema BWANA, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. 15#Mik 4:13; 2 Kor 10:4,5 Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. 16#Yer 51:2 Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli. 17Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, BWANA, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. 18#Isa 35:6,7; Zab 107:35 Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.
19Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja; 20#Ayu 12:9 ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa BWANA ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba.
Ubatili wa miungu
21Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo. 22Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; watuoneshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye. 23#Kum 18:22; Yer 10:5 Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu; naam, tendeni mema au tendeni mabaya, ili tujipime, tukaone pamoja. 24Tazameni, ninyi si kitu, tena kazi yenu si kitu; awachaguaye ninyi ni chukizo.
25 # Ezr 1:2 Nimemwinua mtu toka kaskazini, naye amekuja; toka maawio ya jua amekuja anitajaye jina langu; naye atawakanyaga watawala kama akanyagaye matope, na kama mfinyanzi apondaye udongo. 26Ni nani aliyeihubiri habari tokea mwanzo, tupate kuijua? Na tokea zamani, tupate kusema, Yeye ni mwenye haki? Naam, hapana hata mmoja aliyetujulisha; naam, hapana hata mmoja aliyetuonesha; naam, hapana hata mmoja aliyesikia maneno yenu. 27Mimi kwanza nitauambia Sayuni, Tazama; hawa ndio; nami nitampa Yerusalemu mletaji wa habari njema. 28#Isa 63:5; Dan 2:10 Na nitazamapo, hapana mtu, hata katika watu hao hapana mshauri mmoja, ambaye, nikimwuliza, aweza kunijibu neno. 29Tazama, hao wote ni ubatili; kazi zao si kitu; sanamu zao ni upepo mtupu.

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 41: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha