Zaburi 75:1-10
Zaburi 75:1-10 BHN
Tunakushukuru, ee Mungu, tunakushukuru! Tunatangaza ukuu wa jina lako na kusimulia juu ya matendo yako makuu. Mungu asema: “Mimi nimeweka wakati maalumu! Wakati huo nitahukumu kwa haki. Nchi ikitetemeka na vyote vilivyomo, mimi ndiye ninayeitegemeza misingi yake. Nawaambia wenye kiburi: ‘Acheni kujigamba’; na waovu: ‘Msioteshe pembe za kiburi! Msijione kuwa watu wa maana sana, wala kusema maneno ya majivuno.’” Hukumu haitoki mashariki au magharibi; wala haitoki nyikani au mlimani. Mungu mwenyewe ndiye hakimu; humshusha mmoja na kumkweza mwingine. Mwenyezi-Mungu, anashika kikombe mkononi, kimejaa divai kali ya hasira yake; anaimimina na waovu wote wanainywa; naam, wanainywa mpaka tone la mwisho. Lakini mimi nitafurahi milele, nitamwimbia sifa Mungu wa Yakobo. Atavunja nguvu zote za watu waovu; lakini nguvu za waadilifu ataziimarisha.