Zaburi 135:1-12
Zaburi 135:1-12 BHN
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu, msifuni enyi watumishi wake. Msifuni enyi mkaao katika nyumba yake, ukumbini mwa nyumba ya Mungu wetu! Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; mtukuzeni kwa nyimbo maana inafaa. Mwenyezi-Mungu amemchagua Yakobo kuwa wake, nyinyi watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe. Najua hakika kuwa Mwenyezi-Mungu ni mkuu; Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote. Mwenyezi-Mungu hufanya chochote anachotaka, mbinguni, duniani, baharini na vilindini. Ndiye aletaye mawingu kutoka mipaka ya dunia; afanyaye gharika kuu kwa umeme, na kuvumisha upepo kutoka ghala zake. Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza huko Misri, wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika. Ndiye aliyefanya ishara na maajabu kwako, ee Misri, dhidi ya Farao na maofisa wake wote. Ndiye aliyeyaangamiza mataifa mengi, akawaua wafalme wenye nguvu: Kina Sihoni mfalme wa Waamori, Ogu mfalme wa Bashani, na wafalme wote wa Kanaani. Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake; naam, ziwe riziki ya watu wake Israeli.