Zaburi 135:1-12
Zaburi 135:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu, msifuni enyi watumishi wake. Msifuni enyi mkaao katika nyumba yake, ukumbini mwa nyumba ya Mungu wetu! Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; mtukuzeni kwa nyimbo maana inafaa. Mwenyezi-Mungu amemchagua Yakobo kuwa wake, nyinyi watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe. Najua hakika kuwa Mwenyezi-Mungu ni mkuu; Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote. Mwenyezi-Mungu hufanya chochote anachotaka, mbinguni, duniani, baharini na vilindini. Ndiye aletaye mawingu kutoka mipaka ya dunia; afanyaye gharika kuu kwa umeme, na kuvumisha upepo kutoka ghala zake. Ndiye aliyewaua wazaliwa wa kwanza huko Misri, wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika. Ndiye aliyefanya ishara na maajabu kwako, ee Misri, dhidi ya Farao na maofisa wake wote. Ndiye aliyeyaangamiza mataifa mengi, akawaua wafalme wenye nguvu: Kina Sihoni mfalme wa Waamori, Ogu mfalme wa Bashani, na wafalme wote wa Kanaani. Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake; naam, ziwe riziki ya watu wake Israeli.
Zaburi 135:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haleluya. Lisifuni jina la BWANA, Enyi watumishi wa BWANA, sifuni. Ninyi msimamao nyumbani mwa BWANA, Nyuani mwa nyumba ya Mungu wenu. Msifuni BWANA kwa kuwa BWANA ni mwema, Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza. Kwa sababu BWANA amejichagulia Yakobo, Na Israeli, wawe watu wake hasa. Maana najua ya kuwa BWANA ni mkuu, Na Bwana wetu yuko juu ya miungu yote. BWANA amefanya kila lililompendeza, Katika mbingu na katika nchi, Katika bahari na katika vilindi vyote. Ndiye apandishaye mvuke toka miisho ya nchi; Huifanyia mvua umeme; Hutoa upepo katika ghala zake. Aliwapiga wazaliwa wa kwanza wa Misri, Wa wanadamu na wa wanyama. Alituma ishara na maajabu kati yako, Ee Misri, Juu ya Farao na watumishi wake wote. Aliwapiga mataifa mengi, Akawaua wafalme wenye nguvu; Sihoni, mfalme wa Waamori, Na Ogu, mfalme wa Bashani, Na falme zote za Kanaani. Akaitoa nchi yao iwe urithi, Urithi wa Israeli watu wake.
Zaburi 135:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haleluya. Lisifuni jina la BWANA, Enyi watumishi wa BWANA, sifuni. Ninyi msimamao nyumbani mwa BWANA, Nyuani mwa nyumba ya Mungu wenu. Msifuni BWANA kwa kuwa BWANA ni mwema, Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza. Kwa sababu BWANA amejichagulia Yakobo, Na Israeli, wawe watu wake hasa. Maana najua mimi ya kuwa BWANA ni mkuu, Na Bwana wetu yu juu ya miungu yote. BWANA amefanya kila lililompendeza, Katika mbingu na katika nchi, Katika bahari na katika vilindi vyote. Ndiye apandishaye mvuke toka miisho ya nchi; Huifanyia mvua umeme; Hutoa upepo katika hazina zake. Aliwapiga wazaliwa wa kwanza wa Misri, Wa wanadamu na wa wanyama. Alipeleka ishara na maajabu kati yako, Ee Misri, Juu ya Farao na watumishi wake wote. Aliwapiga mataifa mengi, Akawaua wafalme wenye nguvu; Sihoni, mfalme wa Waamori, Na Ogu, mfalme wa Bashani, Na falme zote za Kanaani. Akaitoa nchi yao iwe urithi, Urithi wa Israeli watu wake.
Zaburi 135:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Msifuni BWANA. Lisifuni jina la BWANA, msifuni, enyi watumishi wa BWANA, ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya BWANA, katika nyua za nyumba ya Mungu wetu. Msifuni BWANA, kwa kuwa BWANA ni mwema, liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza. Kwa maana BWANA amemchagua Yakobo kuwa wake mwenyewe, Israeli kuwa hazina yake ya pekee. Ninajua ya kuwa BWANA ni mkuu, kwamba Bwana wetu ni mkuu kuliko miungu yote. BWANA hufanya lolote apendalo, mbinguni na duniani, katika bahari na vilindi vyake vyote. Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia; hupeleka miali ya radi pamoja na mvua na huleta upepo kutoka ghala zake. Alimuua mzaliwa wa kwanza wa Misri, mzaliwa wa kwanza wa wanadamu na wanyama. Alipeleka ishara zake na maajabu katikati yako, ee Misri, dhidi ya Farao na watumishi wake wote. Aliyapiga mataifa mengi, na akaua wafalme wenye nguvu: Mfalme Sihoni na Waamori, Ogu mfalme wa Bashani na wafalme wote wa Kanaani: akatoa nchi yao kuwa urithi, urithi kwa watu wake Israeli.