Methali 19:13-22
Methali 19:13-22 BHN
Mtoto mpumbavu ni balaa kwa baba yake; na ugomvi wa mke ni kama matone ya mvua yasiyoisha. Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa wazee wake, lakini mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi-Mungu. Uzembe ni kama usingizi mzito; mtu mvivu atateseka kwa njaa. Anayeshika amri anasalimisha maisha yake; anayepuuza agizo atakufa. Anayemsaidia maskini anamkopesha Mwenyezi-Mungu; Mwenyezi-Mungu atamlipa kwa tendo lake jema. Mrudi mwanao kungali bado na tumaini, lakini usimwadhibu kiasi cha kumwangamiza. Mtu wa hasira kali lazima apate adhabu; ukimwachia mara moja itakubidi kumwachia tena. Sikiliza shauri na kupokea mafundisho, upate hekima ya kukufaa siku zijazo. Kichwani mwa mtu mna mipango mingi, lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika. Kinachotakiwa kwa mtu ni uaminifu; afadhali mtu maskini kuliko mtu mwongo.