Methali 19:13-22
Methali 19:13-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtoto mpumbavu ni balaa kwa baba yake; na ugomvi wa mke ni kama matone ya mvua yasiyoisha. Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa wazee wake, lakini mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi-Mungu. Uzembe ni kama usingizi mzito; mtu mvivu atateseka kwa njaa. Anayeshika amri anasalimisha maisha yake; anayepuuza agizo atakufa. Anayemsaidia maskini anamkopesha Mwenyezi-Mungu; Mwenyezi-Mungu atamlipa kwa tendo lake jema. Mrudi mwanao kungali bado na tumaini, lakini usimwadhibu kiasi cha kumwangamiza. Mtu wa hasira kali lazima apate adhabu; ukimwachia mara moja itakubidi kumwachia tena. Sikiliza shauri na kupokea mafundisho, upate hekima ya kukufaa siku zijazo. Kichwani mwa mtu mna mipango mingi, lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika. Kinachotakiwa kwa mtu ni uaminifu; afadhali mtu maskini kuliko mtu mwongo.
Methali 19:13-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kudondoka kwa matone daima. Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA. Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa. Yeye aihifadhiye amri huihifadhi nafsi yake; Bali yeye asiyeziangalia njia zake atakufa. Amhurumiaye maskini humkopesha BWANA; Naye atamlipa kwa tendo lake jema. Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake. Mtu wa hasira nyingi atachukua adhabu yake, Maana ujapomwokoa huna budi kufanya tena. Sikiliza mashauri, ukapokee mafundisho, Upate kuwa na hekima siku zako za mwisho. Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la BWANA ndilo litakalosimama. Haja ya mwanadamu ni hisani yake; Ni afadhali maskini kuliko mwongo.
Methali 19:13-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima. Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA. Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa. Yeye aihifadhiye amri huihifadhi nafsi yake; Bali yeye asiyeziangalia njia zake atakufa. Amhurumiaye maskini humkopesha BWANA; Naye atamlipa kwa tendo lake jema. Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake. Mtu wa hasira nyingi atachukua adhabu yake, Maana ujapomwokoa huna budi kufanya tena. Sikiliza mashauri, ukapokee mafundisho, Upate kuwa na hekima siku zako za mwisho. Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la BWANA ndilo litakalosimama. Haja ya mwanadamu ni hisani yake; Ni afadhali maskini kuliko mwongo.
Methali 19:13-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye, naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha. Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi, bali mke mwenye busara hutoka kwa BWANA. Uvivu huleta usingizi mzito, naye mtu mzembe huona njaa. Yeye ambaye hutii mafundisho huulinda uhai wake, bali yeye anayezidharau njia zake atakufa. Yeye amhurumiaye maskini humkopesha BWANA, naye atamtuza kwa aliyotenda. Mkanye mwanao, kwa maana kufanya hivyo kuna tumaini, usiwe mshirika katika mauti yake. Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake, kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena. Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho, nawe mwishoni utakuwa na hekima. Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu, lakini kusudi la BWANA ndilo litakalosimama. Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho, afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.