Yeremia 49:1-6
Yeremia 49:1-6 BHN
Kuhusu Waamoni. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Je, Israeli hana watoto? Je, hana warithi? Mbona basi mungu Milkomu amemiliki Gadi na watu wake kufanya makao yao mijini mwake? Basi, wakati unakuja kweli, siku zaja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, ambapo nitavumisha sauti ya vita dhidi ya Raba mji wa Waamoni. Raba utakuwa rundo la uharibifu, vijiji vyake vitateketezwa moto; ndipo Israeli atakapowamiliki wale waliomiliki. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Ombolezeni, enyi watu wa Heshboni, maana mji wa Ai umeharibiwa! Lieni enyi binti za Raba! Jifungeni mavazi ya gunia viunoni ombolezeni na kukimbia huko na huko uani! Maana mungu Milkomu atapelekwa uhamishoni, pamoja na makuhani wake na watumishi wake. Mbona mnajivunia mabonde yenu, enyi msioamini, watu mliotegemea mali zenu, mkisema: ‘Nani atathubutu kupigana nasi?’ Basi, mimi nitawaleteeni vitisho kutoka kwa jirani zenu wote, nanyi mtafukuzwa nje kila mtu kivyake, bila mtu wa kuwakusanya wakimbizi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Lakini baadaye nitawarudishia Waamoni fanaka yao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”