Yeremia 49:1-6
Yeremia 49:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Kuhusu Waamoni. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Je, Israeli hana watoto? Je, hana warithi? Mbona basi mungu Milkomu amemiliki Gadi na watu wake kufanya makao yao mijini mwake? Basi, wakati unakuja kweli, siku zaja, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, ambapo nitavumisha sauti ya vita dhidi ya Raba mji wa Waamoni. Raba utakuwa rundo la uharibifu, vijiji vyake vitateketezwa moto; ndipo Israeli atakapowamiliki wale waliomiliki. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Ombolezeni, enyi watu wa Heshboni, maana mji wa Ai umeharibiwa! Lieni enyi binti za Raba! Jifungeni mavazi ya gunia viunoni ombolezeni na kukimbia huko na huko uani! Maana mungu Milkomu atapelekwa uhamishoni, pamoja na makuhani wake na watumishi wake. Mbona mnajivunia mabonde yenu, enyi msioamini, watu mliotegemea mali zenu, mkisema: ‘Nani atathubutu kupigana nasi?’ Basi, mimi nitawaleteeni vitisho kutoka kwa jirani zenu wote, nanyi mtafukuzwa nje kila mtu kivyake, bila mtu wa kuwakusanya wakimbizi. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Lakini baadaye nitawarudishia Waamoni fanaka yao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Yeremia 49:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuhusu wana wa Amoni. BWANA asema hivi, Je, Israeli hana wana? Je! Hana mrithi? Basi, mbona Malkamu anamiliki Gadi, na watu wake wanakaa katika miji yake? Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya kishindo cha vita kisikike juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema BWANA. Omboleza, Ee Heshboni, Kwa maana Ai umeangamizwa; Lieni, enyi binti za Raba, Mjivike nguo za magunia; Ombolezeni, mkipiga mbio Huko na huko kati ya maboma; Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa, Makuhani wake na wakuu wake pamoja. Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijia? Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, BWANA wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao. Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema BWANA.
Yeremia 49:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Habari za wana wa Amoni. BWANA asema hivi, Je, Israeli hana wana? Je! Hana mrithi? Basi, mbona Malkamu anamiliki Gadi, na watu wake wanakaa katika miji yake? Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakaposikizisha mshindo wa vita juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema BWANA. Piga yowe, Ee Heshboni, Kwa maana Ai umeangamizwa; Lieni, enyi binti za Raba, Mjivike nguo za magunia; Ombolezeni, mkipiga mbio Huko na huko kati ya maboma; Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa, Makuhani wake na wakuu wake pamoja. Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijilia? Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, BWANA wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao. Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema BWANA.
Yeremia 49:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kuhusu Waamoni: Hili ndilo asemalo BWANA: “Je, Israeli hana wana? Je, hana warithi? Kwa nini basi Moleki amechukua milki ya Gadi? Kwa nini watu wake wanaishi katika miji yake? Lakini siku zinakuja,” asema BWANA, “nitakapopiga ukelele wa vita dhidi ya Raba, mji wa Waamoni; utakuwa kilima cha magofu, navyo vijiji vinavyouzunguka vitateketezwa kwa moto. Kisha Israeli atawafukuza wale waliomfukuza,” asema BWANA. “Lia kwa huzuni, ee Heshboni, kwa kuwa Ai umeangamizwa! Pigeni kelele, enyi wakazi wa Raba! Vaeni gunia na kuomboleza, kimbieni hapa na pale ndani ya kuta, kwa kuwa Moleki ataenda uhamishoni, yeye pamoja na makuhani na maafisa wake. Kwa nini unajivunia mabonde yako, kujivunia mabonde yako yaliyozaa sana? Ee binti usiye mwaminifu, unayeutumainia utajiri wako na kusema, ‘Ni nani atakayenishambulia?’ Nitaleta hofu kuu juu yako kutoka kwa wale wote wanaokuzunguka,” asema Bwana, BWANA wa majeshi. “Kila mmoja wenu ataondolewa, wala hakuna hata mmoja atakayekusanya wakimbizi. “Lakini hatimaye, nitarudisha mateka wa Waamoni,” asema BWANA.