Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 32:1-25

Yeremia 32:1-25 SRUV

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, katika mwaka wa kumi wa Sedekia, mfalme wa Yuda, nao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa Nebukadneza. Basi, wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli liliuzunguka Yerusalemu; na Yeremia, nabii, alikuwa amefungwa ndani ya uwanja wa walinzi, uliokuwa katika nyumba ya mfalme wa Yuda. Kwa maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga, akisema, Kwa nini unatabiri, na kusema, BWANA asema hivi, Angalia, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atautwaa; tena, Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona kutoka katika mikono ya Wakaldayo, lakini hakika yake atatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, atanena naye ana kwa ana, na watatazamana macho kwa macho; naye atamchukua Sedekia mpaka Babeli, naye atakuwako huko hadi nitakapomjia, asema BWANA; mjapopigana na Wakaldayo hamtafanikiwa. Yeremia akasema, Neno la BWANA limenijia, kusema, Tazama, Hanameli, mwana wa Shalumu, mjomba wako, atakujia, akisema, Jinunulie shamba langu lililoko Anathothi; maana haki ya ukombozi ni yako, ulinunue. Basi Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akanijia ndani ya ukumbi wa walinzi, sawasawa na lile neno la BWANA, akaniambia, Tafadhali, ulinunue shamba langu lililoko Anathothi, katika nchi ya Benyamini; maana haki ya urithi ni yako, na haki ya ukombozi ni yako; ujinunulie. Ndipo nikajua kama neno hili ni neno la BWANA. Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha. Nami nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga mhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani. Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa mhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi; na ile hati ya kununua nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mbele ya uso wa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, na mbele ya mashahidi wale walioitia sahihi hati ya kununua, mbele ya Wayahudi wote walioketi katika ukumbi wa walinzi. Nami nikamwagiza Baruku mbele yao, nikisema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Twaa hati hizi, hati hii ya kununua, hati hii iliyopigwa mhuri, na hii iliyo wazi pia, ukazitie katika chombo cha udongo, zipate kukaa siku nyingi. Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyumba na mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii. Hata nikiisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, hati ile ya kununua, nilimwomba BWANA, nikisema, Aa! Bwana MUNGU, tazama, wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza; wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, BWANA wa majeshi ndilo jina lake; mkuu wa mashauri, muweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake, wewe uliyeweka ishara na ajabu katika nchi ya Misri hata siku hii ya leo, katika Israeli na kati ya watu wengine; na kujifanyia jina kama ilivyo leo; ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mkuu; ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi itiririkayo maziwa na asali; nao wakaingia, wakaimiliki; lakini hawakuitii sauti yako, wala hawakuenda katika sheria yako; hawakutenda neno lolote katika haya uliyowaagiza wayatende; basi, kwa sababu hii umeleta juu yao mabaya haya yote; angalia maboma haya; wameujia mji huu ili kuutwaa; na mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo wanaopigana nao, kwa sababu ya upanga, na njaa, na tauni; na hayo uliyosema yamekuwa; na, tazama, wewe unayaona. Nawe, Ee Bwana MUNGU, umeniambia, Jinunulie shamba lile kwa fedha, ukawaite mashahidi; iwapo mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo; je! Itakuwaje?

Soma Yeremia 32