Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 1:19-28

1 Samueli 1:19-28 BHN

Kesho yake asubuhi, Elkana na jamaa yake waliamka asubuhi na mapema, na baada ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu, walirudi nyumbani Rama. Elkana akalala na mkewe Hana, naye Mwenyezi-Mungu akamkumbuka. Hivyo Hana akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Hana akamwita mtoto huyo Samueli, kwani alisema, “Nimemwomba kwa Mwenyezi-Mungu.” Elkana na jamaa yake yote wakaenda tena Shilo na kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko ya kila mwaka na kutimiza nadhiri. Lakini safari hii Hana hakwenda, kwani alimwambia hivi mumewe, “Mara mtoto atakapoachishwa kunyonya, nitampeleka ili awekwe mbele ya Mwenyezi-Mungu, abaki huko daima.” Elkana, mumewe, akamjibu, “Fanya unaloona linafaa. Ngojea hadi utakapomwachisha mtoto kunyonya. Mwenyezi-Mungu aifanye nadhiri yako kuwa kweli.” Basi, Hana alibaki nyumbani, akaendelea kumlea mtoto wake hadi alipomwachisha kunyonya. Alipomwachisha kunyonya alimpeleka pamoja na fahali wa miaka mitatu, gunia la unga na kiriba cha divai. Hana alimwingiza mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, naye mtoto alikuwa mdogo tu. Walipokwisha kumchinja yule fahali, walimpeleka mtoto kwa kuhani Eli. Hana akamwambia, “Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyekuwa anasimama mbele yako akimwomba Mwenyezi-Mungu. Nilimwomba anipe mtoto huyu, na yeye alinipa kile nilichomwomba. Kwa sababu hiyo, mimi ninampa Mwenyezi-Mungu mtoto huyu; wakati wote atakapokuwa hai, ametolewa kwa Mwenyezi-Mungu.” Halafu, wakamwabudu Mwenyezi-Mungu hapo.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 1 Samueli 1:19-28

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha