1 Samueli 1:19-28
1 Samueli 1:19-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Kesho yake asubuhi, Elkana na jamaa yake waliamka asubuhi na mapema, na baada ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu, walirudi nyumbani Rama. Elkana akalala na mkewe Hana, naye Mwenyezi-Mungu akamkumbuka. Hivyo Hana akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Hana akamwita mtoto huyo Samueli, kwani alisema, “Nimemwomba kwa Mwenyezi-Mungu.” Elkana na jamaa yake yote wakaenda tena Shilo na kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko ya kila mwaka na kutimiza nadhiri. Lakini safari hii Hana hakwenda, kwani alimwambia hivi mumewe, “Mara mtoto atakapoachishwa kunyonya, nitampeleka ili awekwe mbele ya Mwenyezi-Mungu, abaki huko daima.” Elkana, mumewe, akamjibu, “Fanya unaloona linafaa. Ngojea hadi utakapomwachisha mtoto kunyonya. Mwenyezi-Mungu aifanye nadhiri yako kuwa kweli.” Basi, Hana alibaki nyumbani, akaendelea kumlea mtoto wake hadi alipomwachisha kunyonya. Alipomwachisha kunyonya alimpeleka pamoja na fahali wa miaka mitatu, gunia la unga na kiriba cha divai. Hana alimwingiza mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, naye mtoto alikuwa mdogo tu. Walipokwisha kumchinja yule fahali, walimpeleka mtoto kwa kuhani Eli. Hana akamwambia, “Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyekuwa anasimama mbele yako akimwomba Mwenyezi-Mungu. Nilimwomba anipe mtoto huyu, na yeye alinipa kile nilichomwomba. Kwa sababu hiyo, mimi ninampa Mwenyezi-Mungu mtoto huyu; wakati wote atakapokuwa hai, ametolewa kwa Mwenyezi-Mungu.” Halafu, wakamwabudu Mwenyezi-Mungu hapo.
1 Samueli 1:19-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaomba mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume; akamwita Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA. Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea BWANA dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake. Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa kunyonya, hapo ndipo nitakapomleta, ili awepo mbele za BWANA, akae huko daima. Elkana, mumewe, akamwambia, Haya, fanya uonavyo vema; ngoja hadi utakapomwachisha kunyonya; BWANA na alithibitishe neno lake tu. Basi yule mwanamke akangoja, akamnyonyesha mtoto wake, hadi akamwachisha kunyonya. Naye alipomwachisha kunyonya, akamchukua pamoja naye, na ng'ombe watatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta nyumbani kwa BWANA, huko Shilo; na yule mtoto alikuwa mtoto mdogo. Nao wakamchinja huyo ng'ombe, wakamleta mtoto kwa Eli. Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba BWANA. Niliomba nipewe mtoto huyu; BWANA akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa BWANA mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa BWANA. Naye akamwabudu BWANA huko.
1 Samueli 1:19-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA. Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea BWANA dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake. Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa maziwa, hapo ndipo nitakapomleta, ili ahudhurie mbele za BWANA, akae huko daima. Elkana, mumewe, akamwambia, Haya, fanya uonavyo vema; ngoja hata utakapomwachisha maziwa; BWANA na alithibitishe neno lake tu. Basi yule mwanamke akangoja, akamnyonyesha mtoto wake, hata akamwachisha maziwa. Naye alipokuwa amekwisha kumwachisha maziwa, akamchukua pamoja naye, na ng’ombe watatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta nyumbani kwa BWANA, huko Shilo; na yule mtoto alikuwa mtoto mdogo. Nao wakamchinja huyo ng’ombe, wakamleta mtoto kwa Eli. Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba BWANA. Naliomba nipewe mtoto huyu; BWANA akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa BWANA mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa BWANA. Naye akamwabudu BWANA huko.
1 Samueli 1:19-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kesho yake asubuhi na mapema waliamka wakaabudu mbele za BWANA na kisha wakarudi nyumbani kwao huko Rama. Elikana akakutana kimwili na mkewe Hana, naye BWANA akamkumbuka. Hivyo wakati ulipotimia, Hana akapata mimba na akamzaa mwana. Hana akamwita jina lake Samweli, akasema, “Kwa kuwa nilimwomba kwa BWANA.” Wakati huyo mtu Elikana alipanda pamoja na jamaa yake yote kutoa dhabihu ya mwaka kwa BWANA na kutimiza nadhiri yake, Hana hakwenda. Alimwambia mume wake, “Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, nitamchukua na kumpeleka mbele za BWANA, naye ataishi huko wakati wote.” Elikana mumewe akamwambia, “Fanya lile unaloona ni bora zaidi kwako. Ukae hapa mpaka utakapomwachisha kunyonya, BWANA na akujalie kutimiza nadhiri yako.” Hivyo huyo mwanamke akakaa nyumbani na kumnyonyesha mwanawe mpaka alipomwachisha kunyonya. Baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, Hana akamchukua huyo mtoto, akiwa mdogo hivyo hivyo, pamoja na fahali wa miaka mitatu, efa ya unga na kiriba cha divai, naye akamleta mtoto kwenye nyumba ya BWANA huko Shilo. Walipokwisha kumchinja yule fahali, wakamleta mtoto kwa Eli, naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwa BWANA. Niliomba mtoto huyu, naye BWANA amenijalia kile nilichomwomba. Hivyo sasa ninamtoa kwa BWANA. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa BWANA.” Naye akamwabudu BWANA huko.