Warumi 4:13-22
Warumi 4:13-22 SRUV
Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Abrahamu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika. Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa. Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazawa wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Abrahamu; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia moja), na hali ya utasa wa tumbo lake Sara. Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutoamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.