Mithali 18:7-16
Mithali 18:7-16 SRUV
Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake. Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharibifu. Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake. Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili? Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa. Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu.