Methali 18:7-16
Methali 18:7-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Kinywa cha mpumbavu humwangamiza mwenyewe; mdomo wake ni mtego wa kumnasa yeye mwenyewe. Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo kitamu; ambacho hushuka moja kwa moja mpaka tumboni. Mtu mvivu kazini mwake ni ndugu yake mharibifu. Jina la Mwenyezi-Mungu ni mnara imara; mwadilifu huukimbilia akawa salama. Lakini tajiri hudhani mali ni ngome yake; anafikiri hayo ni ukuta mrefu unaomlinda. Majivuno ya moyoni huleta maangamizi, lakini unyenyekevu huleta heshima. Kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu. Roho ya mtu huweza kustahimili ugonjwa, lakini ukiwa umevunjika moyo, utastahimilije? Mtu mwenye akili hujipatia maarifa, sikio la mwenye busara hutafuta maarifa. Zawadi humfungulia mtu milango; huweza kumfikisha mtu mbele ya mkuu.
Methali 18:7-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake. Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharibifu. Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake. Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili? Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa. Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu.
Methali 18:7-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake. Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu. Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake. Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake. Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili? Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa. Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu.
Methali 18:7-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake. Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu; huingia sehemu za ndani sana za mtu. Mtu aliye mlegevu katika kazi yake ni ndugu na yule anayeharibu. Jina la BWANA ni ngome imara, wenye haki huikimbilia na kuwa salama. Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome, wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa. Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi, bali unyenyekevu hutangulia heshima. Yeye ajibuye kabla ya kusikiliza, huo ni upumbavu wake na aibu yake. Roho ya mtu itastahimili katika ugonjwa bali roho iliyovunjika ni nani awezaye kuistahimili? Moyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa, masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa. Zawadi humfungulia njia mtoaji, nayo humleta mbele ya wakuu.