Mithali 13:1-9
Mithali 13:1-9 SRUV
Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu. Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. Kuna mtu anayejitajirisha, lakini hana kitu; Kuna anayejifanya kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. Fidia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lolote. Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.