Methali 13:1-9
Methali 13:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtoto mwenye hekima husikia maagizo ya baba yake, lakini mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu mwema hupata mema kutokana na maneno yake, lakini wadanganyifu huishi kwa ukatili. Achungaye mdomo wake huyahifadhi maisha yake, anayeropoka ovyo hujiletea maangamizi. Mvivu hutamani lakini hapati chochote, hali mwenye bidii hujaliwa riziki kwa wingi. Mwadilifu huuchukia uongo, lakini mwovu hutenda kwa aibu na fedheha. Uadilifu huwalinda wenye mwenendo mnyofu, lakini dhambi huwaangusha waovu. Baadhi hujidai kuwa matajiri kumbe hawana kitu; wengine hujiona kuwa maskini hali wana mali tele. Fidia ya mtu ni mali yake, lakini maskini hana cha kutishwa. Mwadilifu hungaa kama taa iwakayo vizuri, lakini waovu ni kama taa inayozimika.
Methali 13:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu. Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. Kuna mtu anayejitajirisha, lakini hana kitu; Kuna anayejifanya kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. Fidia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lolote. Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.
Methali 13:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu. Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote. Nuru ya mwenye haki yang’aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.
Methali 13:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye, bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Kutoka tunda la midomo yake, mtu hufurahia mambo mema, bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri. Yeye alindaye midomo yake hulinda nafsi yake, bali yeye asemaye kwa haraka ataangamia. Mvivu hutamani sana na hapati kitu, bali nafsi ya mwenye bidii hutoshelezwa kikamilifu. Mwenye haki huchukia uongo, bali waovu huleta aibu na fedheha. Haki humlinda mtu mwadilifu, bali uovu humwangusha mwenye dhambi. Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote; mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi. Utajiri wa mtu unaweza kukomboa maisha yake, bali mtu maskini hasikii kitisho. Nuru ya mwenye haki hungʼaa sana, bali taa ya mwovu itazimwa.