Hesabu 13:1-25
Hesabu 13:1-25 SRUV
Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia, Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila la baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao. Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na BWANA; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli. Na majina yao ni haya; katika kabila la Reubeni, Shamua mwana Zakuri. Katika kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori. Katika kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Katika kabila la Isakari, Igali mwana wa Yusufu. Katika kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni Katika kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu. Katika kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi. Katika kabila la Yusufu, yaani, katika kabila la Manase, Gadi mwana wa Susi. Katika kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali. Katika kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. Katika kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. Katika kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua. Musa akawatuma ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani, mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kama ni wenye nguvu au dhaifu, kama ni wengi au wachache; na nchi wanayoikaa kama ni nzuri au mbaya na kama wanakaa katika kambi au katika ngome; nayo nchi ni ya namna gani, kama ni nchi ya utajiri au ya umaskini; kama ina misitu au haina. Kuweni na mioyo ujasiri, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza. Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hadi Rehobu, mpaka kuingia Hamathi. Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini. Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli. Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arubaini.