Hesabu 13:1-25
Hesabu 13:1-25 NENO
BWANA akamwambia Musa, “Watume baadhi ya watu wakaipeleleze nchi ya Kanaani, ninayowapa Waisraeli. Kutoka kwa kila kabila la baba zao, tuma mwanaume aliye mmoja wa viongozi wao.” Hivyo kwa agizo la BWANA Musa akawatuma kutoka Jangwa la Parani. Wote walikuwa viongozi wa Waisraeli. Haya ndiyo majina yao: kutoka kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri; kutoka kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori; kutoka kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune; kutoka kabila la Isakari, Igali mwana wa Yusufu; kutoka kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni; kutoka kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu; kutoka kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi, kutoka kabila la Manase (kabila la Yusufu), Gadi mwana wa Susi; kutoka kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali; kutoka kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli; kutoka kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi; kutoka kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Haya ndiyo majina ya watu ambao Musa aliwatuma kuipeleleza nchi. (Musa akampa Hoshea mwana wa Nuni jina Yoshua.) Musa alipowatuma wakaipeleleze Kanaani, alisema, “Pandeni kupitia Negebu, mwende hadi nchi ya vilima. Mwone nchi ni ya namna gani, na kama watu wanaoishi humo wana nguvu au ni wadhaifu, iwapo ni wachache au wengi. Wanaishi katika nchi ya namna gani? Je, ni nzuri au mbaya? Wanaishi katika miji ya namna gani? Je, haina kuta au ngome? Ardhi ikoje? Ina rutuba au la? Je, kuna miti ndani yake au la? Jitahidini kadiri mnavyoweza kuleta baadhi ya matunda ya nchi.” (Ulikuwa msimu wa kuiva zabibu za kwanza.) Hivyo wakapanda na kuipeleleza nchi kutoka Jangwa la Sini hadi Rehobu, kuelekea Lebo-Hamathi. Wakapanda kupitia Negebu hadi wakafika Hebroni, mahali ambapo Ahimani, Sheshai na Talmai, wazao wa Anaki, waliishi. (Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko Misri.) Walipofika katika Bonde la Eshkoli, walikata tawi lililokuwa na kishada kimoja cha zabibu. Wawili wao wakalichukua lile tawi kwenye mti, pamoja na komamanga na tini. Eneo lile likaitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya kile kishada cha zabibu ambacho Waisraeli walikikata huko. Baada ya siku arobaini, wakarudi kutoka kuipeleleza nchi.