Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 13:1-25

Hesabu 13:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tuma watu waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani ambayo ninawapa wana wa Israeli. Utatuma mtu mmoja kutoka katika kila kabila, na mtu huyo lazima awe kiongozi katika kabila lake.” Basi, kwa mujibu wa agizo la Mwenyezi-Mungu, Mose akatuma watu kutoka jangwa la Parani. Watu wote waliotumwa walikuwa viongozi wa makabila mbalimbali ya wana wa Israeli. Ifuatayo ndiyo orodha ya majina ya watu hao: Kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri. Kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori. Kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Kabila la Isakari, Igali mwana wa Yosefu. Kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni. Kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu. Kabila la Zebuluni, Gadieli mwana wa Sodi. Kabila la Yosefu (yaani kabila la Manase), Gadi mwana wa Susi. Kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali. Kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. Kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. Kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Haya ndiyo majina ya watu ambao Mose aliwatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani. Mose alimpa Hoshea mwana wa Nuni jina jipya, akamwita Yoshua. Alipowatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani, Mose aliwaambia: “Nendeni juu kule Negebu, hadi kwenye nchi ya milima, mkaipeleleze nchi ilivyo. Chunguzeni pia kama watu wanaoishi humo ni wenye nguvu au dhaifu, wengi au wachache. Pelelezeni kama nchi hiyo ni nzuri au mbaya, na kama miji wanamoishi ni kambi au ni nyumba zilizozungukwa na ngome. Chunguzeni pia kama nchi yenyewe ni tajiri au maskini, ina miti au haina. Muwe na mioyo ya ujasiri na mnaporudi chukueni baadhi ya matunda ya nchi hiyo.” Hayo yalikuwa majira ya zabibu zianzapo kuiva. Basi, watu hao wakaenda na kuipeleleza nchi toka jangwa la Sini hadi Rehobu, karibu na njia ya kuingilia Hamathi. Walikwenda hadi Negebu wakapita mpaka mji wa Hebroni. Humo waliwakuta Waahimani, Washeshai na Watalmai, wazawa wa Anaki. (Mji wa Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko nchini Misri). Walipofika katika Bonde la Eshkoli, watu hao walikata shada la mzabibu lililokuwa na matunda mengi nalo lilibebwa na watu wawili juu ya mti. Walichukua pia makomamanga kadhaa na tini. Mahali hapo paliitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya shada ambalo watu hao wa Israeli walikata kutoka mahali hapo. Baada ya kuipeleleza nchi kwa muda wa siku arubaini, watu hao walirudi.

Shirikisha
Soma Hesabu 13

Hesabu 13:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia, Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila la baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao. Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na BWANA; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli. Na majina yao ni haya; katika kabila la Reubeni, Shamua mwana Zakuri. Katika kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori. Katika kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Katika kabila la Isakari, Igali mwana wa Yusufu. Katika kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni Katika kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu. Katika kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi. Katika kabila la Yusufu, yaani, katika kabila la Manase, Gadi mwana wa Susi. Katika kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali. Katika kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. Katika kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. Katika kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua. Musa akawatuma ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani, mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kama ni wenye nguvu au dhaifu, kama ni wengi au wachache; na nchi wanayoikaa kama ni nzuri au mbaya na kama wanakaa katika kambi au katika ngome; nayo nchi ni ya namna gani, kama ni nchi ya utajiri au ya umaskini; kama ina misitu au haina. Kuweni na mioyo ujasiri, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza. Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hadi Rehobu, mpaka kuingia Hamathi. Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini. Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli. Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arubaini.

Shirikisha
Soma Hesabu 13

Hesabu 13:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia, Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao. Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na BWANA; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli. Na majina yao ni haya; katika kabila ya Reubeni, Shamua mwana Zakuri. Katika kabila ya Simeoni, Shafati mwana wa Hori. Katika kabila ya Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Katika kabila ya Isakari, Igali mwana wa Yusufu. Katika kabila ya Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni Katika kabila ya Benyamini, Palti mwana wa Rafu. Katika kabila ya Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi. Katika kabila ya Yusufu, yaani, katika kabila ya Manase, Gadi mwana wa Susi. Katika kabila ya Dani, Amieli mwana wa Gemali. Katika kabila ya Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. Katika kabila ya Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. Katika kabila ya Gadi, Geueli mwana wa Maki. Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua. Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani, mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi; na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome; nayo nchi ni ya namna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa, kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na moyo mkuu, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza. Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi. Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini. Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli. Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini.

Shirikisha
Soma Hesabu 13

Hesabu 13:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

BWANA akamwambia Musa, “Watume baadhi ya watu wakaipeleleze nchi ya Kanaani, ninayowapa Waisraeli. Kutoka kwa kila kabila la baba zao, tuma mwanaume aliye mmoja wa viongozi wao.” Hivyo kwa agizo la BWANA Musa akawatuma kutoka Jangwa la Parani. Wote walikuwa viongozi wa Waisraeli. Haya ndiyo majina yao: kutoka kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri; kutoka kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori; kutoka kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune; kutoka kabila la Isakari, Igali mwana wa Yusufu; kutoka kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni; kutoka kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu; kutoka kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi, kutoka kabila la Manase (kabila la Yusufu), Gadi mwana wa Susi; kutoka kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali; kutoka kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli; kutoka kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi; kutoka kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Haya ndiyo majina ya watu ambao Musa aliwatuma kuipeleleza nchi. (Musa akampa Hoshea mwana wa Nuni jina Yoshua.) Musa alipowatuma wakaipeleleze Kanaani, alisema, “Pandeni kupitia Negebu, mwende hadi nchi ya vilima. Mwone nchi ni ya namna gani, na kama watu wanaoishi humo wana nguvu au ni wadhaifu, iwapo ni wachache au wengi. Wanaishi katika nchi ya namna gani? Je, ni nzuri au mbaya? Wanaishi katika miji ya namna gani? Je, haina kuta au ngome? Ardhi ikoje? Ina rutuba au la? Je, kuna miti ndani yake au la? Jitahidini kadiri mnavyoweza kuleta baadhi ya matunda ya nchi.” (Ulikuwa msimu wa kuiva zabibu za kwanza.) Hivyo wakapanda na kuipeleleza nchi kutoka Jangwa la Sini hadi Rehobu, kuelekea Lebo-Hamathi. Wakapanda kupitia Negebu hadi wakafika Hebroni, mahali ambapo Ahimani, Sheshai na Talmai, wazao wa Anaki, waliishi. (Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko Misri.) Walipofika katika Bonde la Eshkoli, walikata tawi lililokuwa na kishada kimoja cha zabibu. Wawili wao wakalichukua lile tawi kwenye mti, pamoja na komamanga na tini. Eneo lile likaitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya kile kishada cha zabibu ambacho Waisraeli walikikata huko. Baada ya siku arobaini, wakarudi kutoka kuipeleleza nchi.

Shirikisha
Soma Hesabu 13