Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 31:1-14

Yeremia 31:1-14 SRUV

Wakati huo, asema BWANA, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu. BWANA asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha. BWANA alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu. Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi. Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake. Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni, tukaende Sayuni, kwa BWANA, Mungu wetu. Maana BWANA asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee BWANA, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli. Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia, na pamoja nao watakuja walio vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na uchungu wa kuzaa; watarudi huko, jeshi kubwa. Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawapitisha kwenye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu. Lisikieni neno la BWANA, enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali; mkaseme, Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake. Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye. Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, wataukimbilia wema wa BWANA, nafaka, na divai, na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng'ombe; na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji; wala hawatahuzunika tena kabisa. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, na vijana na wazee pamoja; maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao. Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono, na watu wangu watashiba kwa wema wangu, asema BWANA.

Soma Yeremia 31

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha