Waamuzi 12:1-7
Waamuzi 12:1-7 SRUV
Kisha watu wa Efraimu walikusanyika na kuvuka hadi Zafoni; wakamwambia Yeftha, Kwa nini ulivuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaichoma nyumba yako juu yako. Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na mzozo mkali na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao. Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatarisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, BWANA naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami? Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, na kukaa kati ya Efraimu na Manase. Nao Wagileadi wakavitwaa vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha kila mmoja wa watoro walitoroka Efraimu aliposema “Niache nivuke”, hao watu wa Gileadi walimuuliza, “Je! Wewe ni Mwefraimu?” Alijibu, la; ndipo walipomwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka watu elfu arubaini na mbili wa Efraimu wakati huo. Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo.