Waamuzi 12:1-7
Waamuzi 12:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Watu wa kabila la Efraimu walikusanyika, wakavuka mto Yordani wakafika huko Zafoni. Kisha wakamwambia Yeftha, “Kwa nini hukutuita tuende pamoja nawe kupigana na Waamoni? Sasa tutaichoma nyumba yako nawe mwenyewe ndani yake.” Yeftha akawaambia, “Mimi pamoja na watu wangu tulikuwa na uadui mkubwa na Waamoni. Niliwaombeni mnisaidie lakini hamkuja kuniokoa. Nilipoona kwamba hamkuja kuniokoa, nilikwenda, roho mkononi, kupigana na Waamoni, naye Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu. Kwa nini sasa mnakuja kupigana na mimi?” Basi, Yeftha akakusanya watu wote wa Gileadi, akapigana na watu wa Efraimu. Watu wa Gileadi wakawashinda watu wa Efraimu. Hawa Waefraimu ndio hao waliokuwa wamesema: “Nyinyi watu wa Gileadi ni wakimbizi wa kabila la Efraimu mliotoka katika kabila la Efraimu mkaenda kwa kabila la Manase.” Kisha watu wakavishika vivuko vya mto Yordani ili kuiziba njia ya watu wa Efraimu. Kila mara alipotokea mkimbizi akaomba kupita huko, watu wa Gileadi walimwuliza, “Je, wewe ni Mwefraimu?” Na kama alijibu, “La,” walimwambia: “Haya tamka neno ‘Shibolethi’” lakini yeye hutamka “Sibolethi,” kwa sababu hakuweza kulitamka sawasawa. Hapo, walimkamata, wakamuua huko kwenye vivuko vya mto Yordani. Watu 42,000 wa Efraimu walipoteza maisha yao wakati huo. Yeftha alikuwa mwamuzi katika Israeli kwa miaka sita. Kisha akafariki, akazikwa huko Gileadi katika mji wake.
Waamuzi 12:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha watu wa Efraimu walikusanyika na kuvuka hadi Zafoni; wakamwambia Yeftha, Kwa nini ulivuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaichoma nyumba yako juu yako. Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na mzozo mkali na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao. Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatarisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, BWANA naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami? Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, na kukaa kati ya Efraimu na Manase. Nao Wagileadi wakavitwaa vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha kila mmoja wa watoro walitoroka Efraimu aliposema “Niache nivuke”, hao watu wa Gileadi walimuuliza, “Je! Wewe ni Mwefraimu?” Alijibu, la; ndipo walipomwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka watu elfu arubaini na mbili wa Efraimu wakati huo. Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo.
Waamuzi 12:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha watu wa Efraimu walikutana pamoja na kupita kwenda upande wa kaskazini; wakamwambia Yeftha, Kwa nini wewe kuvuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaipiga moto nyumba yako juu yako. Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na matata makubwa na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao. Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatirisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, BWANA naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami? Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, mnaokaa kati ya Efraimu, na kati ya Manase. Nao Wagileadi wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha ilikuwa, hapo watoro waliotoroka Efraimu mmojawapo aliposema Niache nivuke, hao watu wa Gileadi wakamwambia, Je! Wewe u Mwefraimu? Kwamba alisema, La; ndipo wakamwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka wakati huo watu arobaini na mbili elfu wa Efraimu. Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo.
Waamuzi 12:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Watu wa Efraimu wakaita majeshi yao, wakavuka kwenda Zafoni. Wakamwambia Yefta, “Kwa nini mmeenda kupigana na Waamoni bila kutuita ili twende pamoja nawe? Basi tutaichoma moto nyumba yako, pamoja nawe ukiwa ndani yake.” Yefta akajibu, “Mimi na watu wangu tulikuwa na ugomvi mkubwa na Waamoni. Ingawa niliwaita, hamkuniokoa kutoka mkono wao. Nilipoona kuwa hamniokoi, nikauhatarisha uhai wangu, nikavuka kupigana na Waamoni. Naye BWANA akanipatia ushindi dhidi yao. Sasa kwa nini mnanijia leo ili kupigana nami?” Ndipo Yefta akakusanya wanaume wa Gileadi pamoja na kupigana na Efraimu. Wagileadi wakawashinda Waefraimu, kwa kuwa Waefraimu walisema, “Ninyi Wagileadi ni waasi mliotoroka toka Efraimu na Manase.” Wagileadi wakaviteka vivuko vya Mto Yordani kuelekea Efraimu. Kisha ilikuwa yeyote aliyenusurika kutoka Efraimu aliposema, “Niache nivuke,” hao wanaume wa Gileadi walimuuliza, “Je wewe ni Mwefraimu?” Akijibu “Hapana,” walimwambia, “Sawa, sema ‘Shibolethi’.” Iwapo alitamka, “Sibolethi”, kwa sababu hakuweza kutamka hilo neno sawasawa, walimkamata na kumuua hapo kwenye vivuko vya Mto Yordani. Waefraimu elfu arobaini na mbili waliuawa wakati huo. Yefta akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa muda wa miaka sita. Kisha Yefta akafa, akazikwa katika mmoja wa miji ya Gileadi.